Sisitizo la Pakistan la kuendelea na misimamo yake dhidi ya Israel

Waziri Mkuu wa Pakistan Muhammad Shahbaz Sharif ameitaja hali ya kutia wasiwasi inayoshuhudiwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kuwa ni changamo kubwa kwa amani na usalama duniani.

Shahbaz Sharif pia amezitaja sera za kichokozi na kivamizi za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi za Palestina na kutochukua hatua jamii ya kimataifa kuwa ndiyo sababu ya kushtadi matatizo ya raia wa Palestina. Waziri Mkuu wa Pakistan amesema katika ujumbe aliotuma kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Wananchi wa Palestina inayoadhimisha kila mwaka tarehe 29 Novemba kwamba: “Wananchi na serikali ya Pakistan wanasisitiza tena uungaji wao mkono usioyumba kwa watu  wa Palestina.” Mwanasiasa huyo wa Pakistan ameeleza kuwa: “Suala hili linatutia wasiwasi sana kuona raia wa Palestina wanaendelea kuteseka kwa zaidi ya miongo saba sasa uvamizi haramu wa utawala wa Israel.” Shahbaz Sharif amelaani mashambulizi ya kinyama ya utawala wa kizayuni huko Ghaza na kueleza kuwa, kupewa kinga utawala huo unaoikalia Quds kwa mabavu kumeutia kiburi  zaidi na hivyo kuzidisha vitendo vyake vya utumiaji mabavu dhidi ya Wapalestina. Kwa msingi huo Wapalestina wataendelea kupata hasara na kukabiliwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za wazi za kukomesha jinai za Israel.

Ujumbe wa wazi wa Waziri Mkuu wa Pakistan katika Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Wananchi wa Palestina unaonyesha kuwa, wanasiasa wanaotawala huko Pakistan katika hali na mazingira yoyote yale hawako tayari kutupilia mbali malengo ya wananchi madhulumu wa Palestina na badala yake kukubali sera za kibaguzi na za maangamizi ya kizazi za utawala wa Kizayuni wa Israel. Huko nyuma pia, Ehsan Iqbal mwakilishi wa ngazi ya juu wa chama cha Muslim League cha Nawaz, ambaye pia ni Waziri wa MIipango wa Pakistan alisema: “Sera ya serikali ya Pakistani iko wazi. “Pakistani kamwe haitaitambua rasmi Israel na daima inawaunga mkono na kushikamana na kaka na dada zake wanaokandamizwa huko Palestina.” Ehsan Iqbal aliyasema hayo katika hotuba yake akizungumzia tetesi kuhusu safari ya ujumbe wa wanaharakati wa amani kutoka kundi la Wapakistan wenye uraia wa Marekani huko Israel.

Harakati za Marekani na utawala wa Kizayuni na washirika wao katika uga wa kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel, ni kielelezo cha njama na mipango ya hadaa inayofanyika kutaka kuhalalisha utawala huo bandia.

Baada ya kuhadaiwa baadhi ya serikali za nchi zilizobakia nyuma kifikra za Kiarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kuamua kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel, maafisa wa serikali za Marekani na Israel, kwa dhana kwamba wamefanikiwa kubadili mitazamo ya mataifa mengi ya duniani, wamefanya jitihada kubwa za kuhakikisha vyombo vya habari vya Wazayuni kutoka huko Israel vinakuwepo kwa wingi katika mashindano ya kandanda ya Kombe la Dunia nchini Qatar. Lengo halisi la Israeli katika jitihada hizo lilikuuwa kuyahadaa mataifa ya dunia. Ni dhahiri kwamba baada ya kuzihadaa serikali za baadhi ya nchi za Kiarabu, wanasiasa hao wa Kizayuni wanafanya juu chini kuyapotosha mataifa ya Kiarabu na kupunguzua uungaji mkono wao kwa taifa la Palestina. Hata hivyo kile kilichoakisiwa na vyombo vya habari vya Israel kutoka Qatar ni chuki na upinzani wa mataifa ya Kiarabu dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Israel.

Wanasiasa wanaotawala huko Islamabad na wananchi Waislamu wa Pakistan daima wamekuwa wakiunga mkono matakwa na mapambano ya wananchi madhulumu wa Palestina. Kuhusiana na suala hilo makumi ya wendesha baiskeli wa Pakistani waliandamana katika mji wa Karachi, makao makuu ya mkoa wa Sindh, ili kuelezea mshikamano wao na watu wa Palestina. Wendesha baiskeli hao waliokuwa wakiimba wimbo wa taifa wa Pakistan na kutoa nara za kulaani ubeberu wa kimataifa, wametangaza hasira na upinzani wao dhidi ya jinai na uhalifu unaofanywa na utawala katili wa Israel na madola ya kibeberu. Washiriki katika kampeni hiyo pia wametangaza kuwa, madola ya kibeberu yanakusudia kuwasahaulisha walimwengu suala muhimu la Ulimwengu wa Kiislamu kwa kuunga mkono njama ya kuanzisha uhusiano baina ya nchi za Waislamu na utawala haramu wa Israel. Hata hivyo Waislamu hawataacha kukitetea kibla chao cha kwanza na watu wanaodhulumiwa wa Palestina.

Mwaka 2020 Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco, zilisaini mpango hatari wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel kwa upatanishi wa Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani. Nchi nyingine za Kiarabu na Kiislamu hazijakaribisha mpango huo muovu kwa kutilia maanani ukweli kwamba, uhusiano wa aina yoyote na utawala wa Kizayuni unakabiliwa na upinzani mkubwa wa mataifa na wananchi.

Licha ya kufeli siasa za kibaguzi za Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina, baadhi ya serikali za nchi zilizohadaiwa za eneo la Magharibi mwa Asia zingali zinahimzwa kushirikiana na utawala ghasibu wa Israel. Hii ni licha ya kwamba ushirikiano kama huo ambao hauungwi mkono na mataifa ya Kiislamu, hautazaa matunda na wala hauwezi kuwa halali. Wakuu wa nchi kama hizo wanajielekeza upande wa kushirikiana na utawala wa Israel ili kupata manufaa ya kibinafsi na ya kifamilia.

Kwa ujumla inatupasa kusema kuwa, kwa kutumia vibaya masuala ya ndani ya Pakistan, katika miezi ya hivi karibuni utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya juhudi maradufu za kuvihimiza baadhi ya vyama vya siasa vya Pakistan vishirikiane na utawala wa Kizayuni kupitia njia ya kuzidisha hitilafu katika safu za vyama hivyo. Pamoja na hayo, njama za wanasiasa wa Israel hadi sasa hazijazaa matunda.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *