Khatibu wa msikiti mtakatifu wa al-Aqswa huko Palestina amesema, wananchi wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu wanaoshuhudia mashindano ya soka ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Qatar wamethibitisha kugonga mwamba mpango mchafu wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.
Samahat Sheikh Ikrima Sabri sambamba na kuashiria msimamo sahihi unaoonyeshwa na Waislamu katika mashindano hayo amesema kuhusiana na mwenendo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel ameeleza kuwa, wananchi wa mataifa ya Kiarabu, Kiislamu na wa mataifa mengine wameonyesha mapenzi yao makubwa kwa taifa la Palestina, msikiti wa al-Aqswa na wakati huo huo kuonyesha chuki na hasira zao kwa maghasibu Wazayuni.
Moja ya matukio ya kuvutia katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar ni kukataa wananchi wa mataifa mbalimbali ya Kiarabu kuhojiwa na vyombo vya habari vya Israel na vilevile kuiunga mkono Palestina dhidi ya utawala huo wa Kizayuni.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeashiria matatizo makubwa yanayowakumba waandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni katika mashindano ya Kombe la Dunia 2022 yanayoendelea hivi sasa nchini Qatar na kuandika, katika mashindano haya tumeelewa ni kiasi gani hatupendwi na tunachukiwa vibaya katika ulimwengu wa Kiarabu.
Mbali na kutangaza uungaji mkono wao kwa Wapalestina, watazamaji wa mashindano ya soka ya Kombe la Dunia la 2022 Qatar hususan kutoka mataifa ya Kiarabu wameyatumia mashindano hayo kudhihirisha pia chuki zao dhidi ya Israel kwa kukataa kuhojiwa na waandishi wa habari kutoka utawala huo dhalimu wa Kizayuni.