Kuzinduliwa kampeni kwenye mitandao ya kijamii yenye alama ya hashtag “Kufeli Uanzishaji Uhusiano na Israel Katika Kombe la Dunia Qatar” kumekaribishwa kwa wingi na wanaharakati wa Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati na nchi zingine za Kiarabu ambao wote wamesisitiza kwa kauli moja kwamba, Kombe la Dunia la Soka nchini Qatar limefichua na kuzima njama ya Imarati ya kueneza mpango wa kuanzisha uhusiano na Wzayuni.
Kampeni hiyo imezinduliwa na ‘Jumuiya ya Imarati ya Muqawama dhidi ya Uanzishaji Uhusiano na utawala wa Kizayuni’ na lengo lake ni kuwasaidia na kuwaunga mkono watu wanaokataa kuwasiliana na vyombo vya habari vya Kizayuni, ambao kwa hatua yao wanawahakikishia walimwengu kuwa, kwa watu wenye sharafu na wanaojiheshimu, kuanzisha uhusiano na utawala bandia wa Israel hakukubaliki.
Kampeni hiyo pia ina madhumuni ya kufichua jinai za utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kulaani wale wanaohimiza na kueneza mpango wa kuanzisha uhusiano na utawala huo wakiongozwa na Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati.
Kwa mujibu wa tovuti ya Emirates Leaks, Jumuiya ya Imarati ya Muqawama dhidi ya Uanzishaji Uhusiano na utawala wa Kizayuni’ imewasifu Waarabu na Waislamu wanaohudhuria mechi za Kombe la Dunia la Soka mjini Doha kwa kukataa kuhojiwa na vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni pembeni ya michuano hiyo ya soka.
Muhammad bin Saqr al-Zaabi, mshauri wa masuala ya kisheria na mpinzani wa mpango wa kuanzisha uhusiano na Israel kutoka Imarati amesema: “kushindwa vibaya sana kwa mchakato wa kuanzisha uhusiano kumethibitisha kuwa wasaliti wanaopigia upatu mpango huo hawapati msukumo wowote zaidi ya uwongo unaoenezwa na vyombo vyao vya habari”.