Vyombo vya mahakama vya Saudi Arabia vimepitisha hukumu ya adhabu ya kifo kwa vijana kadhaa waliowekwa kizuizini ukiwa ni mwendelezo wa utoaji hukumu za kifo kiholela kwa raia wanaoshikiliwa kwa sababu za kiitikadi.
Faili la haki za binadamu la Saudi Arabia limetapakaa damu za watu wasio na hatia hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia wa nchi hiyo, lakini nchi za Magharibi na vyombo vyao vya habari ziko kimya juu ya suala hilo zikionyesha misimamo ya kinafiki na kiundumakuwili.
Duru za masuala ya sheria zimeripoti kuwa, hukumu za adhabu ya kifo zimetolewa kwa Muhammad Al-Tahnoun, Mustafa Abu Shahin, Abdullah Ghazvi na kwamba wafungwa wengine watatu Zuhair Al-Samkhan, Mohammed Al-Musabah na Radhi Al-Shayib wanaoshtakiwa katika kesi ya pamoja nao pia wako hatarini kunyongwa.
Kwa mujibu wa duru hizo, kufuatia kutolewa kwa hukumu hizo, idadi ya watu walio hatarini kunyongwa na utawala wa Aal Saud imefikia 59; na hii ni katika hali ambayo, Riyadh inaendelea kupuuza miito ya kimataifa na ya asasi za kutetea haki za binadamu ya kupinga utekelezwaji kiholela wa adhabu za kifo dhidi ya raia wa nchi hiyo.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, mnamo mwaka uliopita wa 2021 utawala wa Aal Saud uliwanyonga watu 69, mwaka 2020 watu 27 na katika mwaka 2019 ulitekeleza adhabu ya kifo dhidi ya watu 187 nchini humo.
Wakati vyombo vya habari za Magharibi vimenyamazia kimya matukio hayo, jumuiya za kimataifa zimepaza sauti zao na kutangaza kuwa hukumu za vifo zilizotekelezwa nchini Saudi Arabia katika mwaka huu wa 2022 ni mara mbili zaidi ya mwaka wa 2021.
Kutokana na hali hiyo, timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imeanzisha kampeni ya kutaka kusitishwa mara moja utekelezaji wa hukumu ya kifo nchini Saudia.