Katika miezi michache iliyopita, matatizo ya kiuchumi na kijamii katika nchi za Ulaya, hasa Uingereza, yameongezeka na kusababisha maandamano ya kijamii na mikusanyiko katika nchi hizo. Mikusanyiko mingi imekabiliwa na ukandamizaji wa vikosi vya polisi ambavyo vimekuwa vikitumia mkono wa chuma kuwatawanya waandamanaji.
Kuhusiana na suala hilo, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ametetea utendaji kazi wa polisi wa nchi hiyo katika kuwakandamiza waandamanaji ambapo katika kikao chake na wakuu wa polisi amesema: ‘Polisi wa Uingereza wana haki ya kukandamiza maandamano yoyote yasiyo ya kisheria na wana uungaji mkono wa serikali.’
Msimamo wa Waziri Mkuu wa Uingereza unakuja wakati ambao katika miezi ya hivi karibuni, London na miji mingine ya Uingereza imekuwa uwanja wa maandamano ya wananchi wanaopinga hatua na sera za kisiasa na kiuchumi za serikali ya nchi hiyo.
Gharama kubwa ya mafuta, kufilisika viwanda vingi, ongezeko la ukosefu wa ajira, mfumuko usio wa kawaida wa bei na ongezeko kubwa la gharama ya maisha ni baadhi ya mambo ambayo yameiweka Uingereza katika hali mbaya zaidi ya kiuchumi katika nusu karne iliyopita.
Hali hii mbaya imesababisha wananchi wengi wa nchi hiyo kupinga utendaji kazi wa serikali kwa kufanya mikutano, maandamano na mikusanyiko ya hadhara. Katika muktadha huo, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Gordon Brown amesema: Zaidi ya asilimia 70 ya Waingereza wanauchukulia umaskini, ukosefu wa usawa wa kijamii na mfumuko wa bei kuwa mambo muhimu zaidi katika maisha yao.
Hayo yanajiri wakati ambao mikusanyiko mingi ya amani imekabiliwa na ukandamizaji wa jeshi la polisi la Uingereza.
Ukandamizaji huo wa maandamano pia unaonekana katika nchi nyingine za Ulaya kama vile Ujerumani na Ufaransa. Nchini Ufaransa, kuongezeka mzozo wa kiuchumi na kijamii kumeibua maandamano makubwa, kiasi kwamba katika miezi ya hivi karibuni maelfu ya waandamanaji wa nchi hiyo wameingia mitaani, lakini maandamano hayo pia yamekabiliwa na ukandamizaji wa vikosi vya polisi. Kwa mara kadhaa sasa vikosi vya polisi vya Ufaransa vimewashambulia waandamanaji kwa marungu na gesi ya kutoa machozi. Katika ukandamizaji huo wa kinyama, waandamanaji wengi wamejeruhiwa na makumi ya watu wasio na hatia kukamatwa. Kiwango cha mfumuko wa bei nchini Ufaransa kilivunja rekodi ya miaka 37 na kufikia asilimia 6.2 mwezi Oktoba mwaka huu. Hali kama hiyo inaonekana nchini Ujerumani ambapo mikusanyiko ya maandamano ya raia inakandamizwa na polisi bila huruma.
Ukandamizaji huo wa kinyama unaotekelezwa na polisi kwa amri ya watawala unajiri wakati serikali nchi za Magharibi zinadai kutetea haki za binadamu na kuheshimu haki ya uhuru wa kujieleza na kuheshimu haki za raia. Nchi hizo, hasa katika miaka ya hivi karibuni, zimekuwa zikishutumu nchi nyingi duniani kuwa haziheshimu haki za binadamu. Kwa kisingizio hicho madola ya Magharibi yamekuwa yakieneza chuki na kuingilia mambo ya ndani ya nchi zenye misimamo huru. Mfano wa uingiliaji huo ni misimamo ya uhasama ya Uingereza na nchi nyingine za Magharibi katika machafuko ya hivi sasa nchini Iran, ambapo serikali ya Uingereza imewawekea vikwazo maafisa kadhaa wa usalama na polisi wa Iran kwa kisingizio cha kile ilichokiita kukandamiza maandamano ya wananchi nchini.
Mick Wallace, mbunge wa mrengo wa kushoto wa Bunge la Ulaya, huku akikosoa kukamatwa kwa waandamanaji katika nchi zinazodai kutetea uhuru wa kujieleza, amesema: “Hivi sasa, uhuru wa kujieleza barani Ulaya uko hatarini.” Yeyote anayekosoa vita vya Ukraine anakamatwa kwa kutoa maoni yake.
Hivi ndivyo hali ilivyo Marekani na Kanada pia. Licha ya madai yote ya kutetea haki za binadamu, serikali hizo haziko tayari kuvumilia maandamano na upinzani na hutumia jeshi la polisi kukandamiza maandamano kwa mkono wa chuma. Kuhusiana na hilo, Waziri Mkuu wa Kanada Justin Trudeau amesema: ‘Ili kuwakandamiza waandamanaji, polisi watapewa mamlaka yanayohitajika kuwakamata na kuwatoza faini waandamanaji.’
David Freiheit mwanasheria na mtaalamu wa sheria wa Canada, amekosoa sera za Waziri Mkuu wa Kanada Trudeau na kusema: Serikali ya Trudeau inakandamiza maandamano mengi ya amani kwa sababu haikubaliani na yanayosemwa katika maandamano.
Wakati Marekani na nchi za Magharibi zinadai kuheshimu uhuru, demokrasia na haki za binadamu, wao ndio wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu duniani.