Tovuti ya jarida la Marekani la National Interest limegusia vitendo vya kikatili vilivyofanywa na magaidi wa ndani ya Marekani na kusema kuwa, vita vya pili vya ndani vimeanza katika nchi hiyo ya Magharibi.
Katika ripoti yake ya jana (Jumapili), shirika la habari la IRNA limelinukuu jarida hilo la Marekani likisema kuwa, watu waliofanya machafuko walikabiliana na wale waliopinga machafuko hayo pamoja na ukatili uliofanyika kwa kutumia silaha huko Marekani kwa shabaha ya kuonesha Wazungu ni jamii bora kuliko watu wa rangi nyingine, sambamba na misimamo mikali ya kisiasa iliyooneshwa kwenye mitaa na barabara za Marekani yote hayo ni ushahidi wa kuanza vita vya pili vya ndani nchini Marekani.
Vita vya Pili vya Ndani vya Marekani ni istilahi inayotumiwa na baadhi ya wataalamu wa nchi hiyo kuelezea vipindi muhimu vya machafuko ya kisiasa nchini humo.
Vita vya Kwanza vya Ndani ya Marekani vilianza tarehe 12 Aprili 1861 na kuendelea hadi tarehe 9 Mei 1865. Vita hivyo vilitokea baina ya tawala zilizounga mkono Muungano wa Shirikisho (uliojulikana kwa jina la Umoja) na majimbo ya kusini Marekani yaliyokuwa maarufu kwa jina la Kusini ambayo yalitaka kujitenga na ardhi nyingine za Marekani. Sababu kuu ya kutokea vita hivyo ni hali mbaya ya watumwa hususan kutanua wigo wa utumwa huo hadi katika ardhi za Mexico ambazo ndio kwanza zilikuwa zimetekwa na Marekani.
Mwaka 2021, umoja unaojulikana kwa jina la “The Anti-Defamation League” uliripoti kuwa, ugaidi wa ndani ya Marekani umepelekea watu wasiopungua 29 kuuawa katika matukio 19 tofauti nchini humo. Ukitoa mauaji ya watu watatu, mauaji mengine yote yalitokana na siasa kali na chuki dhidi ya watu wa rangi nyingine.