Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kiuchumi wa Hungary amezionya nchi nyingine za Ulaya kwa uamuzi wao wa kuweka kiwango maalumu cha bei ya kununulia mafuta ya Russia na kusisitiza kuwa, uamuzi huo utatoa pigo kubwa zaidi kwa uchumi wa nchi za bara hilo.
Péter Szijjártó amesema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook na kuongeza kuwa, nchi za Ulaya zinapaswa kupigania kuwa na vyanzo vingi tofauti vya nishati badala ya kupunguza bei ya kununulia mafuta ya Russia, kwani kwa kuwa na vyanzo vingi vya kudhamini nishati kwenyewe kutapelekea kupungua bei ya bidhaa hiyo muhimu.
Aidha amesema: Sisi katika kipindi chote cha mazungumzo ya kujadili suala hilo, tulisimama imara kutetea na kulinda maslahi yetu na mwisho tumefanikiwa, kwani Hungary imesamehewa na imetolewa katika mpango huo wa kununua mafuta ya Russia kwa bei iliyoainshwa na Umoja wa Ulaya.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary pia amesema, kwa mara nyingine tumesimama kidete na tumefanikiwa kulinda usalama wa nchi yetu wa kudhamini nishati inayoihitajia.
Lengo la Umoja wa Ulaya la kuweka bei maalumu ya kununulia mafuta ya Russia ni kujaribu kutoa pigo kwa Moscow na kupunguza mno mapato yake yanayotokana na kuuza nje mafuta ghafi.
Hatua hiyo imechukuliwa huku vita vya Ukraine vikikaribia kutoka kwenye mwaka wa 2022 na kuingia mwaka wa 2023. Vita hivyo vilianza tarehe 24 Februari mwaka huu wa 2022.
Nchi za Ulaya zimeweka kiwango cha dola 60 kwa pipa kwa ajili ya kununua mafuta ya Russia, hatua ambayo imelalamikiwa vikali na baadhi ya nchi za bara hilo.
Hayo yamekuja huku Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika taasisi za kimataifa mjini Vienna, Austria, Mikhail Ulyanov, akisema kuwa, kuanzia mwaka ujao Ulaya itaishi bila ya mafuta ya Russia kufuatia hatua yake ya kuainisha bei ya bidhaa hiyo.