Vitisho vya ajabu vya Marekani kwa Russia; ukiacha kutuuzia mafuta tutakuadhibu

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House mapema leo Jumanne ametoa vitisho vya ajabu dhidi ya Moscow baada ya nchi za Magharibi kuainisha bei maalumu ya kununulia mafuta ya Russia, na kusema kuwa hakushangazwa na radiamali iliyooneshwa na Kremlin.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Karine Jean-Pierre akisema hayo mapema leo na kuongeza kuwa, iwapo Russia itaacha kuziuzia mafuta nchi za Magharibi kwa bei iliyoainishwa na Marekani, basi ijiandae kupigwa faini.

Msemaji huyo wa Ikulu ya Marekani amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, bei iliyoainishwa hivi sasa itakuwa inabadilika muda wote kwani lengo ni kuizuia Russia isinufaike zaidi na vita vya Ukraine.

Amerudia vitisho vyake akisema, iwapo Russia itakataa kuziuzia nchi za Magharibi mafuta yake baada ya kutekelezwa mpango huo wa kununua nishati hiyo kwa bei isiyozidi dola 60 kwa pipa, basi Moscow itakumbwa na matokeo mabaya sana.

Hata hivyo wataalamu wa mambo wanasema kuwa, matamshi hayo ya msemaji wa Ikulu ya Marekani ni ya kutapatapa na ya mfamaji hasa baada ya viongozi wa Russia kutangaza wazi kuwa, hawatoiuzia mafuta, nchi yoyote itakayoshiriki kwenye mpango huo wa kibeberu wa madola ya Magharibi.

Siku chache zilizopita, Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika taasisi za kimataifa mjini Vienna, Austria, Mikhail Ulyanov, alisema wazi kuwa, kuanzia mwaka ujao wa 2023, nchi za Ulaya zitaishi bila ya mafuta ya Russia kufuatia hatua yao ya kuainisha bei ya kununulia bidhaa hiyo bila ya ridhaa ya Moscow.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *