Mazungumzo ya amani ya Congo mjini Nairobi yaakhirishwa kufungwa, waasi watoka mkutanoni

Sherehe za kufunga mazungumzo ya wiki nzima ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ziliongoza mazungumzo ya amani jijini Nairobi, Kenya ziliakhirishwa jana Jumatatu kutokana na mipango duni.

Wajumbe ambao ni pamoja na wawakilishi kutoka makundi makubwa ya waasi na waathirika wa vita vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walitoka nje ya mkutano huo dakika chache baada ya kuanza kwa madai ya kutolipwa posho zao.

Uhuru Kenyatta, rais mstaafu wa Kenya ambaye ndiye Mratibu wa Masuala ya Amani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jana aliakhirisha sherehe za kufungwa mazungumzo ya amani hadi leo Jumanne, na kuwakemea vikali waandaaji wa mkutano huo kwa mipango yao duni.

Katika sehemu moja ya matamshi yake, Kenyatta alisema: “Ningependa kuakhirisha mkutano huu na naomba tukutane hapa kesho. Tunajua, tuna fedha za kutosha, na najua hivyo kwa sababu nilikuwa miongoni mwa watu waliopata fedha za kusaidia kuleta amani DRC.”

Pia amesema: “Kwa waandaaji: Amani si kitu cha kuchezea. Kesho waandaaji wataleta pesa ambazo zilikuwa zimegawiwa ipasavyo kwa washiriki wote wa mchakato huu.”

Mazungumzo ya amani kati ya pande mbalimbali zinazohusika na mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yalihusisha mashauriano kati ya makundi yenye silaha ya mashariki mwa nchi hiyo na viongozi wa serikali za kieneo, mashirika ya kiraia na wadau wengine, kwa lengo la kutafuta suluhu endelevu za migogoro ya miaka mingi ya nchi hiyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *