Zaidi ya taasisi 100 za kutetea haki za binadamu zimeitaka Marekani ihitimishe himaya na uungaji mkono wake kwa utawala wa Saudi Arabia ambao umeendelea kufanya mauaji huko nchini Yemen.
Asasi na taasisi hizo zimewaandikia barua Wabunge wa Marekani ambao wana jukumu la kutunga sheria na kuwataka waunge mkono muswada wa mamlaka ya kivita unaotaka kusitishwa ushiriki wa Marekani katika vita huko Yemen.
Sehemu nyingine ya barua hiyo, inataka Marekani isitishe himaya na uungaji mkono wake kwa Saudia katika vita dhidi ya Yemen na kuishajiisha nchi hiyo kushiriki katika mazungumzo ili kuhitimisha vita hivyo vyenye maafa makubwa.
Joe Biden ambaye wakati wa kampeni za kuwania urais aliahidi kusitisha uungaji mkono wa nchi hiyo kwa vita vya Saudi Arabia na washirika wake huko Yemen amekiuka ahadi yake hiyo baada ya kuingia madarakani.
Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa, mwezi Machi 2015 ilianzisha vita dhidi ya Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa nchi kavu, baharini na anga.
Vita vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen hadi sasa vimeuwa maelfu ya raia wasio na hatia na kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine, huku mamilioni ya Wayemeni wakilazimika kuwa wakimbizi.
Ingawa muungano huo ulianzisha vita dhidi ya Yemen kwa madai ya kuunga mkono serikali iliyojiuzulu ya Abd Rabu Mansour Hadi, lakini baada ya kupita muda ilibainika wazi kuwa muungano huo na waungaji mkono wake wa Magharibi na Wazayuni ulikuwa na mpango ulioainishwa awali wa kuigawa Yemen kwa msingi wa maslahi ya wanachama wake na hasa Saudia na Imarati.