Hatua mpya za nchi za Magharibi za kuzuia matangazo ya Press TV; nembo ya vita vya mseto dhidi ya Iran

Shirika la huduma za satalaiti la Intelsat la Ufaransa limetangaza kukata matangazo ya televisheni ya Press TV ya Iran wiki chache baada ya vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya televisheni hii ambayo hurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiingereza duniani kote.

Umoja wa Ulaya hivi karibuni, kwa kisingizo cha eti kuunga mkono demokrasia, iliweka vikwazo dhidi ya Press TV na baadhi ya watu pamoja na taasisi kadhaa nchini Iran.

Televisheni ya Press TV katika miaka ya hivi karibuni, kwa visingizio kadhaa, imekuwa ikishinikizwa sana na mashirika yanayotoa huduma za kurusha matangazo kwa njia ya sataliti.

Hatua ya Eutelsat inakiuka mikataba ya kimataifa na uhuru wa vyombo vya habari na pia ni kinyume cha madai ya madola ya Magharibi kuhusu uhuru wa maoni na vyombo vya habari.

Katika hatua nyingine pia hivi karibuni Marekani nayo ilimuwekea vikwazo mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) pamoja na wakurugenzi na waandishi habari kadhaa wa shirika hili.

Swali ambalo linaibuka kuhusu hatua hii ya uhasama ya shirika la Kifaransa la Eutelsat ni hili, je ni kwa nini madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kwa upande moja yanadai kutetea uhuru wa maoni na kuunga mkono uhuru wa vyombo vya habari lakini wakati huo huo yanaweka vikwazo dhidi ya vyombo mbali mbali vya habari huru amabavyo vinapinga sera za Magharibi.

Abdul al Qais, mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa anasema: “Uamuzi wa  shirika la Ufaransa la Eutelsat wa kuondoa televisheni ya Press TV katika satalaiti yake ni ishara ya wazi kuwa televisheni hii ya Iran ina ushawishi mkubwa na imeweza kupata ushindi dhidi ya mrengo wa shari duniani.

Katika vikwazo vya hivi karibuni vya nchi za Ulaya dhidi ya Iran ambavyo vimekuwa vikitekelezwa kwa awamu kadhaa, kile ambacho kimewashangaza wengi ni kuwekea vikwazo kanali ya televisheni ya Press TV ya lugha ya Kiingereza.

Kwa muda wa miaka kadhaa sasa Press TV imekuwa ikirusha matangazo yake kwa njia ambayo imevunja ukiritimba wa kihabari wa vyombo vya habari vya Kimagharibi. Kwa hakika Press TV imekuwa ikiakisi matukio ya kimataifa kwa mwelekeo maalumu ambao umeifanya kuwa ‘sauti ya wasio na sauti.’ Nukta hii imekuwa ikiyakasirisha sana madola ya Magharibi ambayo hutumia kila kisingizio kuzuia Press TV kurusha matangazo katika satalaiti na pia katika mitandao ya kijamii kama vile YouTube, Instagram.

Ahmad Nowruzi, Mkuu wa Kitengo cha Matangazo ya Kimataifa cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye pia ni mkurugnezi wa Press TV  amesema ni aibu kuona Eutelsat imeondoa Press TV katika satalaiti na kuongeza kuwa: Huko nyuma pia madola ya Magharibi yaliwahi kuchukua hatua za kuzuia matangazo wa televisheni za Iran katika satalaiti na hivyo hatua ya hivi karibuni ya Eutelsat si mpya.

Nchi za Ulaya ambazo zinashirikiana na Marekani zimekuwa zikichukua hatua zilizo dhidi ya nara za uhuru wa maoni na uhuru wa vyombo vya  habari ili kuzuia msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutangazwa duniani, hasa kuhusu ghasia na fujo za hivi karibuni Iran. Hii ndio sababu ya vikwazo vya hivi karibuni dhidi ya Press TV hatua ambayo imefuatiwa na kusimamishwa matangazo ya televisheni hii katika satalaiti ya Eutelsat.

Hatua ya kuzuia matangazo ya Press TV imechukuliwa katika hali ambayo televisheni nyingi za satalaiti zinazorusha matangazo kwa lugha ya Kifarsi na kwa bajeti ya madola ya Magharibi na baadhi ya madola yanayopinga Mapinduzi ya Kiislamu katika eneo, hasa Saudi Arabia, zimekuwa zikirusha matangazo yao yaliyo dhidi ya Iran bila matatizo yoyote. Miongozni mwa televisheni hizo zilizo dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ni ‘Iran International’ ambayo kwa bajeti ya Saudi Arabia na kwa maelekezo ya Uingereza, imekuwa ikieneza propaganda na hadaa pamoja na harakati nyingine haribifu dhidi ya Iran.

Vyombo hivyo vya habari vimekuwa vikiunga mkono ghasia, fujo na ugaidi nchini Iran kwa uhuru kamili na kwa himaya ya madola ya Magharibi. Si tu kuwa vyombo hivyo vya habari vinaunga mkono waibua fujo bali hata vimekuwa vikitoa mafunzo kwa wafanya ghasia ili kuendeleza machafuko nchini Iran.

Madola ya Ulaya ambayo yanadai kutetea haki za binadamu Iran yameruhusu televiseni hizo kuendesha shughuli zao dhidi ya Iran na hivyo ni wazi kuwa malengo yao ni kuendeleza chuki dhidi ya Iran.

Kwa hakika nukta hiyo inaashiria kuendelea sera za undumakuwuli za nchi za Magharibi kuhusu masuala kama vile ugaidi, haki za binadamu na uhuru wa maoni na vyombo vya habari.

Hali kadhalika kuzuia matangazo ya Press TV katika satalaiti ya Eutelsat ni mfano mwingine wa nchi za Magharibi kuogopa vyombo huru vya habari na hasa  vya Iran. Ni wazi kuwa hatua mpya dhidi ya Press TV ni katika fremu ya ‘vita vya mseto’ dhidi ya Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *