Hizbullah yahimiza kuchaguliwa rais mpya wa Lebanon haraka iwezekanavyo

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Shekhe Naeem Qassim ametilia mkazo ulazima wa kuchaguliwa rais mpya wa nchi hiyo haraka iwezekanavyo.

Katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Shekhe Naeem Qassim amesema: “katika kipindi hiki, sisi ndani ya Hizbullah tunatilia mkazo masuala mawili makuu na muhimu; la kwanza ni kwamba rais achaguliwe haraka iwezekanavyo na suala la pili pia ni kuwa inampasa aende sambamba na matakwa na mahitaji ya watu”.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza na kufafanua zaidi kwa kusema: “rais ajaye wa Lebanon inapasa awe na sifa tatu kuu, ambazo ni ” kusimamia mpango wa kuokoa uchumi”, “kuweza kuwa na mawasiliano na ushirikiano na pande zote mbili zilizoko kwenye medani” na vilevile “asiwe mtu mchochezi, bali afanye kazi kwa utulivu kwa ajili ya kushughulikia masuala yanayozusha tofauti na hitilafu”.

Kauli hiyo ya Shekhe Naeem Qassim imetolewa katika hali ambayo katika kikao chake cha siku ya Alkhamisi, bunge la Lebanon lilishindwa kwa mara ya tisa kumchagua rais mpya kutokana na kutofikiwa mwafaka kati ya mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo.

Akizungumza kabla ya kikao hicho, Spika wa Bunge Nabih Berri alisema, Lebanon haiwezi kustahamili kwa zaidi ya wiki zingine kadhaa hali iliyopo hivi sasa na kwamba kipaumbele cha kwanza nchini ni kumchagua rais mpya.

Urais wa miaka sita wa aliyekuwa rais wa Lebanon Michel Aoun ulimalizikaOktoba 31. Na licha ya kufanya vikao tisa, Bunge la Lebanon limeshindwa hadi sasa kumchagua rais mpya, na kuifanya hali ya kisiasa ya nchi hiyo iwe tata na tete zaidi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *