Safari ya Rais wa China nchini Saudi Arabia

Rais Xi Jin Ping wa China ambaye amefanya ziara nchini Saudi Arabia mbali na kusaini mapatano ya pamoja ya ushirikiano wa kimkakati, amesaini pia hati 34 za mapatano kwa lengo la kustawisha ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji kati ya nchi mbili.

Rais Xi Jin Ping ametathmini umuhimu wa ziara yake nchini Saudi Arabia na kueleza kuwa “ziara yake hiyo ni sawa na kuanza zama mpya katika uhusiano wa China na Ulimwengu wa Kiarabu. Hii ina maana kuwa, Beijing katika miongo ijayo imekusudia kustafidi na suhula na uwezo mkubwa wa kibiashara na uwekezaji wa nchi za Kiarabu na hasa Saudi Arabia. Suala muhimu katika uwanja huo ni kuendelea kuhakikishiwa upatikanaji wa mafuta ya Saudia.”

China ni nchi inayonunua kwa wingi mafuta ya Saudi Arabia; na kwa sababu hiyo inahesabiwa pia kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Riyadh. Pamoja na hayo, moja ya wasiwasi mkuu wa China khususan katika ushindani baina yake na Marekani ni kukabiliwa na tishio la kufikiwa na mafuta hayo ya Saudia; hatua ambayo inaweza kuathiri vikali sekta ya uzalishaji ya China.

Bruce Riddle wa Taasisi ya nchini Marekani ya Think Tank ya Berkins anaamini kuhusiana na hilo kwamba: “hata kama China inataka kuwa na uhusiano mzuri na wa kiwango cha juu na Saudia lakini inajua vyema kuhusu vigingi na vizuizi vya nchi hiyo. Hii ni kwa sababu uhusiano wa kistratejia kati ya Marekani na Saudi Arabia hauwezi kukengeukwa huku Saudia ikinunua silaha na zana zake za kijeshi kutoka Marekani.”

Mazungumzo ya Rais Xi na baadhi ya wakuu wa nchi za Kiarabu akiwemo Rais wa Misri yanaweza kutiliwa maanani katika uwanja huo. Aidha  kwa mtazamo wa Rais wa China, fursa za uwekezaji nchini Saudi Arabia pia zinaivutia China, ambapo Saudia inajaribu kutoa baadhi ya fursa kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Kichina pia kuwekeza nchini humo.

Pamoja na hayo, serikali ya China inataraji kwamba katika fremu ya mpango wa kiuchumi na uwekezaji wa barabara na ukanda mmoja itafanikiwa kuzidisha uhusiano wake na  Saudi Arabia katika nyanja zote za kiuchumi na uwekezaji. Kwa mtazamo wa Rais wa China, uhusiano wa Beijing unauhusu Ulimwengu wote wa Kiarabu. Amesema, anadhani kuwa kupanuliwa uhusiano kati ya Chna na Saudi Arabia kutafungua mlango wa kuwepo pia uhusiano na Ulimwengu mzima wa Kiarabu.

Kwa hiyo, kwa kuzingatia ushindani mkubwa wa kibiashara uliopo kati ya nchi mbalimbali ikiwemo Korea ya Kusini na India na Japan na pia nchi za Ulaya kwa ajili ya kupanua uwepo wao kiuchumi na kibiashara kwenye masoko ya kikanda ikiwemo pia uwepo wake katika nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi na Saudia; kwa hakika China haipo katika masoko hayo bila ushindani.

Faisal bin Farhan mchambuzi wa masuala ya eneo la Mashariki ya Kati anazungumzia hilo akisema:” mpango wa Ustawi wa 2030 wa Saudi Arabia kwa ajili ya kuivutia China ni fursa nzuri sana; na yale matarajio ya kistratejia kutoka Saudia yanayotajwa na viongozi wa China yanaweza kuiandalia Beijing fursa nzuri ya kushiriki pakubwa katika masoko hayo.

Ala kulli hal, China ambayo katika mchuano kati yake na Marekani katika miaka ya karibuni imekabiliwa na changamoto inafanya kila iwezalo ili kuwepo pakubwa katika masoko ya Kiarabu khususan nchini Saudia. Suala ambalo linaweza kuipelekea Marekani kuhofia kuwa na ushawishi hasimu wake mkubwa katika uga wa kisiasa, kiuchumi na hata kijeshi duniani.

Wakati huo huo, moja ya nukta za kuzingatia kuhusu suala hilo ni jitihada za China za kuimarisha ushirikiano na nchi za Kiarabu ili kuzuia kuenea harakati za makundi yenye misimamo mikali na wakati huo huo kuzuia hujuma za mitandao ya makundi hayo katika maeneo ya mipaka na ndani ya China. Hii ni kwa sababu China inaamini kuwa, nchi za Magharibi khususan Marekani zinayatumia makundi yenye kufurutu ada kama wenzo wa kutoa pigo kwa usalama wa taifa wa nchi mbalimbali ikiwemo China.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *