Duru za Palestina mapema leo Jumatatu zimetangaza habari ya kuuawa shahidi binti mdogo wa Kipalestina kwenye uvamizi wa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika mji wa Jenin wa Ukingo Magharibi wa Mto Jordan.
Tovuti ya habari ya Falastin al Yaum imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa takriban miaka 15 ameuliwa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi makatili wa Israel mapema leo Jumatatu.
Televisheni ya Aljazeera ya Qatar nayo imelinukuu shirika la Hilal Nyekundi la Palestina likisema kuwa, wanajeshi wa Israel wameuvamia mji wa Jenin wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kumezuka mapambano makali baina yao na wakazi wa mji huo. Wapalestina watatu wamejeruhiwa na wengine wawili wametekwa nyara na wanajeshi hao makatili wa Israel.
Televisheni ya Alalam nayo imemnukuu mwandishi wake akiwa mjini Jenin akiripoti kwamba binti huyo wa miaka 15 wa Kipalestina ameuliwa shahidi kwa kupigwa risasi moja kwa moja na wanajeshi Wazayuni huko Jenin.
Ikumbukwe kuwa kundi kubwa la wanajeshi wa vikosi maalumu vya utawala wa Kizayuni mapema leo Jumatatu wamevamia eneo la mashariki mwa Jenin lakini wamekumbwa na muqawama mkali wa wanamapambano wa Palesitna.
Wanamapambano wa Palestina wamewakaribisha wanajeshi hao Wazayuni kwa maguruneti ya kutengeneza kwa mkono na silaha zao za kujitengezea wenyewe.
Brigedi ya Jenin yaani Kataib al Jenin zimetangaza kuwa, wanamapambano wa brigedi hiyo wameendesha mapambano makali ya kukabiliana na wanajeshi vamizi wa Israel kwenye maeneo yao.