Saudia yazidi kuingilia masuala ya Libya, Bin Salman aonana na Menfi mjini Riyadh

Mkuu wa Baraza la Uongozi la Libya, Mohamed al-Menfi, amekutana na mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman katika mji mkuu wa Riyadh kujadili maendeleo ya kisiasa ya Libya na matarajio ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Taarifa ya ofisi ya al-Menfi imesema kuwa, pande hizo mbili pia zimejadiliana masuala kadhaa yanayohusiana na mzozo wa Libya.

Al-Menfi ndiye aliyealikwa katika mkutano wa kilele wa Waarabu na China katika mji mkuu wa Saudia, Riyadh, siku ya Ijumaa ambapo alitoa mwito kwa Waarabu na Wachina kuunga mkono juhudi za kurejesha utulivu nchini Libya.

Libya yenye utajiri wa mafuta imekumbwa na machafuko tangu 2011 wakati mtawala wa muda mrefu Muammar Gaddafi alipong’olewa madarakani baada ya kukaa madarakani kwa miongo minne.

Hali imekuwa mbaya zaidi tangu mwezi Machi mwaka jana wakati bunge lenye makao yake Mashariki mwa Libya lilipoteua serikali mpya inayoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fathi Bashagha, lakini Waziri Mkuu wa serikali ya Tripoli, Abdul Hamid Dbeibeh, mmoja wa watu wawili wanaodai kuwa ndio watawala wastahiki nchini Libya, anasisitiza kuwa atakabidhi madraka kwa serikali inayoingia madarakani kupitia “bunge lililochaguliwa na wananchi,” na hivyo kuzua hofu kwamba Libya inaweza kurejea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Uingiliaji wa madola ya kigeni kama Saudi Arabia katika masuala ya ndani ya Libya unahesabiwa kuwa ndicho kikwazo kikubwa cha kupatikana utulivu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *