Kanali ya televisheni ya KiKA ya Ujerumani imemfuta kazi Matondo Castlo mwendeshaji wa kipindi cha watoto baada ya kushiriki katika maandamano ya amani katika mji wa Bait Dajan huko mashariki mwa mji wa Nablus.
Uongozi wa Televisheni hiyo ya Ujerumani umemtuhumu Matondo kwamba, ana chuki na utawala wa Kizayuni.
Magazeti ya Ujerumani yameandika taarifa kuhusu kushiriki mtangazaji huyo wa televisheni ya KiKA katika maandamano ya wanaoiunga mkono Palestina na kuchapisha makala chini ya anwani “Tamasha la Uchupaji Mipaka” kwamba: Mtangazaji wa KiKA ameandamana bega kwa bega na wapinzani wa Israel ili kwa njia hiyo kujaribu kuamsha fikra za walio wengi dhidi ya Costlo.
Televisheni ya KiKA pia imetangaza kuwa, imeamua kutoendelea kufanya kazi na Castlo hadi masuala yote kuhusu kadhia hiyo yatakapopatiwa ufafanuzi. Matondo Castlo alituma ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao nwa kijamii wa Instagram kwamba amefutwa kazi na kanali ya televisheni ya KiKA ambayo ni kituo cha televisheni cha watoto nchini Ujerumani kwa hatua yake ya kushiriki maandamano katika mji wa Beit Dajan karibu na Nablus huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel mwezi Agosti mwaka huu.
Kufutwa kazi mtangazaji wa Kijerumani kwa sababu ya kuunga mkono Wapalestina kwa mara nyingine tena kumeonyesha sura halisi unafiki wa uhuru na kuheshimu haki za binadamu katika ulimwengu wa Magharibi ukiwemo uhuru wa kusema, kutoa maoni na uhuru wa kushiriki katika mikusanyiko mbalimbali. Ujerumani nayo kama yalivyo mataifa mengine ya Ulaya imekuwa ikionyesha misimamo ya kuukosoa utawala ghasaibu wa Israel katika masuala kama kufukuzwa Wapalestina katika makazi na mashamba yao, lakini kimsingi Berlin inahesabiwa kuwa mmoja wa waungaj mkono wakuu wa kifedha na kisiasa wa Tel Aviv.
Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana madola ya Ulaya ikiwemo Ujerumani si tu kwamba, yamekuwa yakipinga hatua yoyote mpya yenye taathira hasi dhidi ya utawala Bandia wa Israel, bali inapotokea masuala kama ngano ya Holocaust kukoselewa na watafiti au wachunguzi wa mambo, huchukua hatua kali kabisa dhidi ya wahusika.
Mfano hai na wa karibuni kabisa ni kadhia ya kufutwa kazi mtangazaji wa kanali ya televisheni ya KiKa ya Ujerumani. Kuhusiana na ushiriki wake katika maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina Castlo ameeleza bayana kwamba: Maandamano hayo yalikuwa ya amani na lengo lake lilikuwa ni kulalamikia hatua za walowezi wa Kizayuni na wanajeshi wa utawala ghasibu unaoikalia Quds kwa mabavu za kuzipora ardhi za Wapalestina. Matondo Castlo ameongeza kuwa: Mimi sikuwa na nia ya kutoa taarifa ya kisiasa na hata sikuchukua msimamo wowote dhidi ya Israel.
Licha ya ufafanuzi huo lakini wakoasoaji wa hatua dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel hukabiliwa na hatua kama iliyochukuliwa dhidi ya mtangazaji huyo ili kutoa funzo kwa watu wengine wenye nia ya kuwaunga mkono Wapalestina. Hii ni katika haali ambayo, hatua za Wajerumani za kuunga mkono utawala dhalimu wa Israel unaotenda jinai kila uchao dhidi ya Wapalestina zimekuwa zikishabikiwa na kuungwa mkono na serikali ya Berlin.
Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa mtangazaji wa televisheni ya Ujerumani kufutwa kazi kwa kosa la kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa. Februari mwaka huu (2022), wafanyakazi saba wa Kiarabu wa Kanali ya Televiasheni ya Deutsche Welle ya Ujerumani akiwemo Farah Maraqa mwandishi habari wa Kipalestina-Kijordan walifutwa kazi kwa kile kilichoelezwa ” kuwa na chuki dhidi ya Uyahudi”. Mahakama moja ya Ujerumani ilitoa hukumu kwamba, kufutwa kazi Farah Maraqa ilikuwa hatua ya kidhulma na kwamba haikuwa na uhalali wa kisheria.