China imesisitiza kuhusu umuhimu wa uhusiano wake wa jadi na kirafiki na Iran, ikisema uhusiano wa Beijing na Tehran na uhusiano wake na nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (PGCC) haulengi upande wowote.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin amesema, China na Iran zina urafiki wa jadi
Akizungumza na waandishi habari Jumatatu mjini Bejing, amesema, “China inaunga mkono nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi katika kuboresha uhusiano na Iran kwa kuzingatia kanuni ya urafiki wa ujirani mwema.”
Amesema ziara ijayo ya Makamu Waziri Mkuu Hu Chunhua nchini Iran, itakuwa na mchango chanya katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati wa kina kati ya China na Iran.
Hayo yamekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuiasa China iheshimu mamlaka kamili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran juu ya visiwa vyake vitatu vya eneo la Ghuba ya Uajemi. Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa lugha ya Kichina Jumatatu na kuongeza kuwa, visiwa vitatu hivyo vya Ghuba ya Uajemi ni sehemu ya milele ya ardhi ya Iran.
Amesema: Visiwa vitatu vya Bumusa, Tunb Ndogo, na Tunb Kubwa ni sehemu zisizotenganishika na Iran, na daima vitasalia kuwa milki ya ardhi mama ya Iran. Abdollahian ameongeza kuwa: Iran haishughulishwi na pande nyinginezo ikija katika suala la udharura wa kuheshimiwa milki yake.
Mwandiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa visiwa hivyo vitatu vya Ghuba ya Uajemi ni sehemu za milele za ardhi ya Iran na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitafanya mazungumzo kuhusu mamlaka ya mipaka yake. Msimamo huo wa Amir-Abdollahian ni radiamali kwa taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya kikao cha Rais wa China, Xi Jinping na viongozi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi katika mji mkuu wa Saudia Riyadh tarehe 9 Disemba. Taarifa hiyo ilipinga umiliki wa Iran wa visiwa vyake vitatu vya Bumusa, Tunb Ndogo, na Tunb Kubwa. Maafisa wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba visiwa vitatu hivyo ambavyo Umoja wa Falme za Kiarabu unadai kuwa eti ni milki yake, ni sehemu ya ardhi yake.