Mke na mume raia wa Marekani wanaoishi katika mtaa wa Naguru huko Kampala, mji mkuu wa Uganda wametupwa rumande katika gereza la Luzira, wakikabiliwa na mashitaka ya kumtesa na kumdhalilisha mtoto mdogo wa miaka 10.
Mackenzie Leing Mathias Spencer na mumuwe Nicholas Spencer wanatuhumiwa kumuadhibu na kumfanyia kila aina ya mateso mtoto wao wa kambo mwenye umri wa miaka 10.
Wanandoa hao wa Marekani, kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda, wanadaiwa kumfungia mvulana huyo wa miaka 10 chumbani na kutompeleka shule, huku wakimtesa na kumdhalilisha.
Kwa mujibu wa waraka wa mashitaka uliowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Barabara ya Buganda, wawili hao wanakabiliwa na kesi ya kumtesa mtoto mdogo kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Mateso ya 2012.
Sarah Tusiime Bashaija, Hakimu wa Mahakama hiyo ya Uganda amewasukuma wanandoa hao rumande, ambapo wanatazamiwa kurejeshwa kortini kesho Jumatano kujua iwapo wataachiwa huru kwa dhamana au la.
Christine Tumuhairwe, wakili anayeshirikiana na mlezi wa mtoto huyo wa miaka 10 amesema, mtoto huyo ambaye ana virusi vya HIV alifanyiwa kila aina ya mateso na adhabu na Wamarekani hao eti kutokana na ‘makosa’ aliyoyafanya.
Inaarifiwa kuwa, ingawaje wanandoa hao wa Marekani wana watoto wengine wawili wa kupanga, lakini wamekuwa wakimuonea mvulana huyo wa miaka 10, wakidai kuwa ni mkaidi na ana matatizo ya kiakili.
Watoto wote hao watatu hivi sasa wapo mikononi mwa polisi, wakisubiri kupelekwa katika nyumba nyingine ya kuwahifadhi na kuwasitiri.