Zakzaky: Mauaji ya Zaria ni ishara ya Waislamu wa Nigeria kuwa katika njia sahihi

Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, mauaji ya umati ya Zariya yaliyofanywa na vyombo vya usalama vya nchi hhiyo ni ishara ya wazi kwamba, Waislamu wa taifa hilo wamo katika njia sahihi.

Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema hayo wakati alipokutana na familia za wahanga wa shambulio la wanajeshi wa Nigeria huko Zaria Disemba 2015

Kiongozi huyo wa Kiislamu amesema, hatua za jeshi la Nigeria kama kuwashambulia kwa risasi wanawake wajawazito, watoto na kuwachoma kwa moto wakiwa hai wananchi Waislamu wa Nigeria zinakinzana wazi kabisa na utu na ubinadamu.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria sambamba na kulaani jinai hiyo amesisitiza kuwa, waliotenda jinai hizo hawana kabisa utu na wala hawaheshimu madhehebu na hawakuwa na wasiwasi wowote wakati wa kutenda jinai hiyo.

Katika shambulio hilo la Disemba 12, 2015, inakadiriwa wanachama zaidi ya 1,000 wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria, aghalabu wakiwa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na jeshi la Nigeria. Miongoni mwa waliouawa walikuwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Katika siku iliyofuata, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Husseiniyah ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria.

Wakati huo huo, shughuli ya kuwakumbuka mashahidi waliouawa na jeshi la Nigeria miaka saba iliyopita katika mji wa Zaria ilifanyika jana katika Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Mah’had ulioko kaskazini mwa Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *