Kwa mara nyingine tena Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio likisisitiza kuwa eneo la Golan linalokaliwa kwa mabavu na Israel ni milki ya Syria, na kwamba Wapalestina ndio wamiliki wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio hilo la kila mwaka kwa kura 159. Azimio hilo limepasishwa kwa anwani ya: “Mamlaka ya Kudumu wa watu wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zikiwemo Quds na mamlaka ya Wasyria huko Golan inayokaliwa kwa mabavu”.
Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limesisitiza haki zisizoweza kupingika za watu wa Syria huko Golan inayokaliwa kwa mabavu na za wananchi wa Palestina kuhusu maliasili zao zikiwemo ardhi, maji na rasilimali za nishati.
Azimio hilo la Umoja wa Mataifa limeutaka utawala ghasibu wa Israel ukomeshe unyonyaji au uharibifu wa maliasili katika eneo la Golan inayokaliwa kwa mabavu na katika ardhi za Palestina na kusimamisha vitendo vyote vinavyodhuru mazingira vikiwemo vitendo vya walowezi wa Kizayuni wa Israel.
Miiniko ya Golan ni eneo muhimu sana na la kistratijia la Syria, ambalo lilikaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967 na tangu wakati huo Wasyria wamekuwa wakifanya jitihada za kulikomboa.