Rais Paul Kagame wa Rwanda ameikosoa vikali Marekani kwa kuishinikiza serikali ya Kigali imuachie huru Paul Rusesabagina, nyota wa filamu ya “Hotel Rwanda” aliyegeuka na kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Kigali.
Akizungumza mjini Washington pambizoni mwa Mkutano wa Marekani na Afrika, Kagame amesema Rwanda haitamruhusu yoyote kuishinikiza nchi hiyo kufanya jambo linalogusa maisha ya Wanyarwanda.
Rais Kagame amehoji, “Rwanda imuachie huru Rusesabagina kwa msingi gani? Kwa kuwa ni mashuhuri na ni mkazi wa kudumu wa Marekani?”
Rais wa Rwanda amekosoa mwito huo wa Washington wa kutaka mkosoaji wake huyo aachiwe huru akihoji zaidi kwa kuuliza, “Kuachiwa kwake huru (Rusesabagina) kutakuwa na maana gani kwa wenzake 20 waliohukumiwa pamoja?”
Septemba mwaka jana, Mahakama Kuu ya Rwanda ilimhukumu Rusesabagina kifungo cha miaka 25 jela baada ya kumpata na hatia ya kujihusisha na kundi la waasi linalotuhumiwa kuhusika na mashambulio ya umwagaji damu ya utumiaji bunduki, maguruneti na uchomaji moto nchini humo katika miaka ya 2018 na 2019.
Jaji Beatrice Mukamurenzi wa korti hiyo alisema, Rusesabagina aliunda shirika la kigaidi lililoishambulia Rwanda, na akachangia kifedha pia kufadhili harakati za kigaidi.
Hata hivyo waungaji mkono wa ‘shujaa’ huyo wa filamu inayoitwa ‘Hotel Rwanda’ walisema faili la Rusesabagina ilikuwa kesi ya kimaonyesho na iliyochochewa na sababu za kisiasa.
Ikumbukwa kuwa, si Rusesabagina wala mawakili wanaomtetea walifika mahakamani wakati hukumu iliyotolewa dhidi yake iliposomwa mnamo Septemba mwaka jana 2021.