Kuanzisha uhusiano wa kawaida na Saudi Arabia; kipaumbele cha Netanyahu katika sera zake za kigeni

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel aliyepewa jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri la Israel amegusia katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika Rasmi la Habari la Saudia kuhusiana na uhusiano wa Riyadh na Tel-Aviv.

Netanyahu amewahi kuwa Waziri Mkuu wa utawala bandia wa Israel kuanzia 2009-2021 mtawalia na katika kipindi hicho alichukua hatua nyingi na kufanya juhudi kadha wa kadha ili kuhakikisha kwamba, kunaanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya utawala huo na taifa la Saudi Arabia.

Mwaka 2020 juhudi za Netanyahuu zilizaa matunda ambapo mataifa manne ya Kiarabu ya Imarati, Bahrain, Morocco na Sudan yalitilia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo unaotenda jinai kila uchao dhidi ya Wapalestina. Baada ya kuwa nje ya ulingo wa siasa za Israel kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, hatimaye mwezi uliopita, Benjamin Netanyahu alipewa jukumu la kuunda baraza la mawaziri baada ya uchaguzi wa Bunge.

Kuanzisha mataifa mengine ya Kiarabu uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ni jambo ambalo lipo katika ajenda za Netanyahu. Inaonekana kuwa, suala la kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Saudi Arabia na Israel ni katika mambo yanayopewa kipaumbe na Netanyahu. Kadhalika matamshi ya baadhi ya viongozi wa Saudia pia yanaashiria kwamba, wanachukua hatua kuelekea kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Hivi karibuni Adel al-Jubeir, Waziri Mshauri Katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Saudi Arabia sambamba na kukiri kukaribia kutangazwa wazi kuweko uhusiano baina ya Riyadh na Tel Aviv alitangaza kuwa, uhusiano wa pande mbili unaelekea upande wa mapatano, ingawa jambo hili linahitajia muda zaidi.

Hii kwamba, baada ya Netanyahu kupewa jukumu la kuunda serikali mpya ya Israel katika mahojiano ya kwanza tu anafanya na Kanali ya Televisheni ya al-Arabia ya Saudia ni ishara ya wazi ya kuweko azma na irada imara ya pande mbili ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao. Kanali ta Televisheni ya al-Arabia ni chombo rasmi cha Saudia. Matamshi ya Netanyahu pia aliyoyatoa katika mahojiano hayo yana ishara nyingine.

Netanyahu alisisitiza juu ya kuweko umuhimu mkubwa wa kuanzishwa uhusiano na kawaida baina ya Israel na Saudia na kueleza kwamba, katika muda usio mrefu Tel Aviv na Riyadh zitaanzisha uhusiano wa kawaida baina yao.

Jambo jingine ni kuwa, Netanyahu akiwa na lengo la kuikinaisha Saudia aliikosoa serikali ya Marekani sambamba na kulalamikia utendaji wa serikali ya Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden kuhusiana na Saudia. Netanyahu alisema pia kuwa, muungano wa kijadi baina ya Marekani na Saudi Arabia na mataifa mengine unapaswa kuimarishwa na kuongeza kuwa: Kuhusiana na kadhia hii hakupaswi kuweko suala la kubadilisha msimamo kwa kipindi fulani au mabadiliko makubwa ya msimamo, kwani ninadhani kwamba, muungano huu ni mhimili wa uthabiti katika eneo letu.

Matamshi hayo ya Netanyahu yanaashiria mpasuko baina ya Marekani na Saudia ulioibuka katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibu baada ya kuingia madarakani Rais Joe Biden

Licha ya kuwa hadi sasa hakuna uhusiano rasmi baina ya Israel na Saudi Arabia, lakini pande hizo mbili hususan kuanzia mwaka 2020 zimechukua hatua katika mkondo wa kupanua wigo wa ushirikiano wao. Kuanzishwa uhusiano wa baina ya Imarati na Bahrain kulifanyika kwa baraka na ridhaa ya Saudia. Serikali ya Riyadh imefungua anga yake kwa ajili ya ndege za Israel. Si hayo tu, bali kumekuweko na habari za kufanyika safari za baadhi ya viongozi wa Kizayuni huko Saudia.

Kile ambacho hadi sasa kimeifanya Saudia isitangaze kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel ni hofu yake kwa radiamali ya fikra za waliowengi na kupoteza nafasi iliyonayo katika ulimwengu wa Kiislamu.

Fainali za mashindano ya kandanda ya Kombe la Dunia huko nchini Qatar zimethibitisha kwamba, fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiarabu zina chuki kubwa na utawala bandia wa Israel. Wananchi wa mataifa mbalimbali kama Saudi Arabia, Tunisia na Morocco walioko nchini Qatar kushuhudia mashindano ya soka ya Kombe la Dunia mbali na kuonyesha chuki zao kwa Israel wamekuwa wakitangaza wazi himaya na uungaji mkono wao kwa Palestina.

Katika Mashindano hayo dunia ya Soka mwaka huu wa 2022 huko Qatar, watazamaji wa nchi mbalimbali na hasa wa nchi za Kiarabu wamekataa kuhojiwa na vyombo vya habari na maripota wa Israel na wamekuwa wakionyesha uungaji mkono wao kwa Palestina wakati mechi mbalimbali zikifanyika.

Hivi karibuuni gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth liliashiria matatizo makubwa yanayowakumba waandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni katika mashindano ya Kombe la Dunia 2022 yanayoendelea hivi sasa nchini Qatar na kuandika, katika mashindano haya tumeelewa ni kiasi gani hatupendwi na tunachukiwa vibaya katika ulimwengu wa Kiarabu.

Licha ya kuweko chuki hiyo kubwa lakini inaonekana kuwa, utawala wa Aal Saud ukiwa mbioni kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel unafanya juhudi za hatua kwa hatua na kwa kusoma alama za nyakati.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *