Makundi ya muqawama ya Palestina yamelaani mauaji ya mandugu wawili wa Kipalestina katika mji wa Nablus, kaskazini mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesikitishwa na mauaji ya vijana hao wa Kipalestina yaliyofanywa na walowezi wa Kizayuni jana usiku mjini Nablus na kusisitiza kuwa, wanamuqawama watalipiza kisasi cha ukatili huo.
Taarifa ya Hamas imesema: Tunakabiliwa na wimbi la jinai za kila uchao kutoka kwa Wazayuni. Muqawama utaendelea kuwa chaguo bora la watu wetu katika kukabiliana na jinai na chokochoko za walowezi wa Kizayuni.
Harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu imesisitiza kuwa, damu za mashahidi wa Kipalestina zitaendelea kuwa laana na kuwaandama maadui, askari na walowezi wao katika kila barabara na kichochoro cha ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa, mandugu wawili wa Kipalestina Mohammad na Muhannad Yousef Muteir waliokuwa wakiishi katika kambi ya wakimbizi ya Qalandiya kaskazini mwa mji wa Quds waliuawa shahidi jana usiku kwa kugongwa na gari kwa makusudi na walowezi wa Kizayuni mjini Nablus.
Hamas sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia na marafiki wa vijana hao wa Kipalestina waliouawa shahidi usiku wa kuamkia leo, wametoa mwito kwa Wapalestina kutoa jibu kali kwa uhaini huo wa Wazayuni maghasibu.
Hii ni katika hali ambayo, ripoti ya kila wiki ya Ulinzi wa Raia iliyochapishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) huko Palestina, imesema wanajeshi wa Israel wamewaua kwa risasi Wapalestina 19, wakiwemo watoto watatu, katika matukio tofauti katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kati ya Novemba 22 na Disemba 11.