Mfalme wa Abdallah wa Jordan: Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya waibua fujo

Mfalme wa Jordan amechukua msimamo mkali kufuatia maandamano ya wananchi yanayoendelea nchini humo na kuuliwa afisa wa ngazi ya juu wa polisi na kusisitiza kuwa: serikali itachukua hatua kali kwa yoyote atakayewashambulia askari usalama na mali za umma.

Maandamano hayo yalianza katika eneo la al Husseiniya na katika miji mingine kusini mwa Jordan baada ya kupanda bei ya mafuta. Mfalme Abdallah wa Pili wa Jordan amesema katika shughuli ya hitma ya afisa polisi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo ambaye ameuawa katika ghasia na machafuko nchini humo kwamba, hakubaliani na vitendo vya kuwavunjia heshima na kuwashambulia askari usalama ambao wanafanya kazi ya kulinda usalama wa nchi na wa raia.

Mfalme wa Jordan ameongeza kuwa, mashambulizi na hatua za uharibifu zinauweka hatarini usalama wa nchi, na kwamba taasisi  za serikali zitachukua hatua kali kukabiliana na wale wote wanaokiuka sheria za nchi.

Idara ya Usalama ya Jordan imetangaza kuwa, Kanali Abdulrazaq Abdulhafidh Al-Dalabeeh, Naibu Mkuu wa Polisi wa mkoa wa Maan ameuawa kwa kupiga risasi kichwani wakati polisi walipokuwa wakijaribu kutuliza ghasia baada ya kupanda kwa bei ya mafuta.

Wakati huo huo madereva wa magari makubwa na wafanyakazi wa sekta ya usafirishaji nchini Jordan pia wameanza mgomo wakilalamikia kupanda kwa bei ya mafuta. Huku haya yakiripotiwa, watu 44 wametiwa nguvu hadi sasa kwa tuhuma za kuchochea fujo na kuharibu mali za umma katika ghasia zinazoendelea nchini nchini Jordan.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *