Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) anasema urutubishaji wa madini ya urani nchini sasa umefikia kiwango rasmi cha uhalisia wa asilimia 60 kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Majlisi (bunge) mwezi Disemba 2020 inayotaka kuharakishwa maendeleo ya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.
Behrouz Kamalvandi aliyasema hayo katika mkutano wake na wabunge wa Iran siku ya Jumamosi, akizungumzia sheria iliyopewa jina la Mpango wa Mkakati wa Kukabiliana na Vikwazo, ambao unalenga kukabiliana na vikwazo na kuendeleza mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.
Amesema sheria ya bunge “imetoa hali nzuri kwa nchi na leo urutubishaji wetu wa urani umefikia asilimia 60 kwa mujibu wa sheria hii.”
Afisa huyo wa Iran ameongeza kuwa, Iran inafuatilia mipango endelevu ya utafiti na maendeleo huku juhudi zake za kusasisha kizazi kipya cha mashinepewa au centrifuge “zikiwa katika ubora wake.”
Kwa mujibu wa sheria ya bunge, serikali ya Iran inatakiwa kuweka vizuizi katika ukaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kuharakisha maendeleo ya mpango wa nyuklia nje ya mipaka iliyowekwa chini ya makubaliano ya nyuklia ya 2015, ambayo yanajulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA). Kati ya hatua ambazo serikali imetakiwa na bunge kuchukua ni kama vile kukomesha utekelezaji wa hiari wa Itifaki ya Ziada ya Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).
Katika mahojiano na televisheni ya Qatar Al Jazeera mwezi Disemba, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi alisema mpango wa nyuklia wa Iran umepata maendeleo makubwa, na nchi hiyo hivi sasa inarutubisha uranium hadi kiwango cha usafi cha asilimia.
Makubaliano ya nyuklia ya Iran yalitiwa saini mwaka 2015 kati ya Tehran na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na China wakati wa uongozi wa Barack Obama.
Hata hivyo, mrithi wa Obama, Donald Trump aliachana na JCPOA mwezi Mei 2018 na kuiwekea Iran vikwazo vya kikatili. Rais wa sasa Joe Biden alikuwa ameapa kuanzisha tena mazungumzo ya kufufua mpango huo na kuondoa vikwazo vikali vya Marekani. Katika miaka miwili ya uongozi wake, Biden ameshindwa kutimiza ahadi yake na sasa anatishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran.
Iran inashikilia kuwa ni muhimu kwa upande wa pili kutoa dhamana fulani kwamba utafungamana na makubaliano yoyote yatakayoafikiwa ya kuondolewa vikwazo.