Bashagha awataka Walibya kuchukua msimamo mmoja dhidi ya Marekani

Waziri Mkuu aliyeteuliwa na Baraza la Wawakilishi la Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo ametoa wito wa kuwepo msimamo wa pamoja wa nchi yake dhidi ya Marekani.

Ni baada ya maafisa wa serikali za Scotland na Marekani kutangaza Jumapili iliyopita kwamba Mlibya anayetuhumiwa kutengeneza bomu lililosababisha mlipuko wa ndege ya Pan Am kwenye anga ya Lockerbie, Scotland mwaka 1988 yuko kizuizini nchini Marekani.

Fathi Bashagha, ametoa wito kwa watu wa nchi hiyo kuchukua msimamo mmoja wa kitaifa dhidi ya kukamatwa Abu Agila Mohammad Mas’ud Kheir Al-Marimi, raia wa Libya aliyepelekwa Marekani, ambaye anatuhumiwa na Washington kuwa alihusika na kulipuliwa ndege ya PAN AM huko Lockerbie.

Fathi Bashagha amesema Libya haikufurahishwa na kukamatwa na kukabidhiwa kwa Marekani Abu Agila Mohammad katika kesi inayohusiana na kulipuliwa kwa ndege ya PAN AM katika anga ya  Lockerbie.

Huku akieleza kuwa kukabidhiwa Abu Agila kwa Wamarekani kumefanyika kinyume cha sheria na hakukubaliki kabisa, Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Libya ameibebesha dhima Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Abdul Hamid al-Dbeibeh na kusema inawajibika kikamilifu katika kadhia ya al-Rimi.

Ingawa maafisa wa Marekani hawajatoa maelezo kuhusu jinsi Abu Agila alivyokamatwa, lakini ilitangazwa mwezi uliopita kuwa watu wenye silaha walimteka nyara kutoka nyumbani kwake huko Tripoli.

Akijitetea kutokana na lawama za kushirikiana kwake na Marekani katika kadhia ya kukamatwa Abu Agila, al-Dbeibeh ameeleza kuwa, Polisi ya Kimataifa (Interpol) ilitoa waranti wa kumtia nguvuni mshukiwa huyo na kwamba ilikuwa muhimu kwa watu wa Libya kushirikiana katika kadhia hiyo kwa ajili ya maslahi na utulivu wa nchi hiyo.

Ndege ya Pan Am, Boeing 747, iliripuka ikiwa juu ya mji mdogo wa Lockerbie, Scotland, na watu 259 waliokuwemo ndani yake waliuawa na wengine 11 waliaga dunia mahala ndege hiyo ilipoangukia.

Abu Agila Mohammad Mas’ud Kheir Al-Marimi amekamatwa karibu miaka miwili baada ya Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Bill Barr, kutangaza kwa mara ya kwanza kwamba Washington inamtuhumu kuhusika na faili la Lockerbie.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *