Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Saudi Arabia iko tayari kuendeleza mazungumzo na Tehran.
Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter ambapo ameeleza mazungumzo aliyofanya na mawaziri wa mataifa mbalimbali pambizoni mwa mkutano wa Baghdad-2 uliofanyikka huko Amman mji mkuu wa Jordan.
Abdollahian amesema, nimeshiriki katika mkutano wa Baghdad-2 ili nisisitize himaya na uungaji mkono wa nchi yangu kwa Iraq.
Aidha amesema, pambizoni mwa mkutano huo nilikutana na kufanya mazungumzo ya kirafiki na baadhi ya mawaziri wenzangu wa mashauri ya kigeni wa Oman, Qatar, Kuwait na Saudi Arabia..
Hussein Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, katika mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Saudi Arabia, Faisal bin Farhan amemueleza utayari wa nchi yake wa kuendeleza mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu
Mnamo mwaka 2016, Saudi Arabia ilivunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran kwa kisingizio cha kushambuliwa ubalozi wake mjini Tehran na ubalozi wake mdogo mjini Mash’had.
Mvutano wa Saudia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulianza Januari 2016 baada ya Saudia kumnyonga mwanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia Sheikh Nimr Baqir al-Nimr. Kufuatia kunyongwa mwanazuoni huyo, waandamanaji wa Iran waliokuwa na hasira walivamia ubalozi wa Saudia mjini Tehran. Hadi sasa kumefanyika duru tano za mazungumzo baina ya pande mbili katika mji mkuu wa Iraq Baghdad.