Mamia ya wananchi wa Morocco wameandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kupinga mapatano ya kuhuisha uhusiano na utawala wa Kizayuni.
Morocco na utawala wa Kizayuni Disemba 22 mwaka 2020 chini ya usimamizi wa Marekani zilisaini mapatano ya kuanzisha tena uhusiano wa kawaida baina yazo. Mamia ya Wamorocco jana usiku waliandamana katika miji 30 ya nchi hiyo kulalamikia hatua ya nchi yao ya kufikia mapatano hayo na Israel.
Maandamano hayo yamefanyika kwa mwaliko wa muungano wa mashirika na makundi yanayouinga mkono Palestina, zikiwemo harakati 15 za kisiasa, miungano na vituo vya kisheria. Huko Rabat mji mkuu wa Morocco pia wapinzani wa mapatano hayo na Israel walibeba mabango yaliyoandikwa” “Palestina ni amana na mapatano ni usaliti; na mapambano yataendelea hadi kuangamizwa mapatano hayo.” Maandamano hayo ya Wamorocco yalifanyika mbele ya makao makuu ya bunge la nchi hiyo.
Wananchi wa Morocco mara kwa mara wamekuwa wakiandamana na kukusanyika katika maeneo mbalimbali ili kudhihirisha upinzani wao kwa mapatano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa nchi hiyo na utawala haramu wa Kizayuni.