Mashirika makubwa ya misaada yasitisha shughuli Afghanistan baada ya Taliban kupiga marufuku wafanyakazi wa kike

Mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali (NGOs) yamesitisha shughuli zake nchini Afghanistan baada ya serikali ya Taliban kupiga marufuku wanawake kufanya kazi katika mashirika hayo.

Ripoti kutoka nchini humo zinasema kuwa, mashirika kadhaa makubwa ya kigeni yasiyo ya kiserikali nchini Afghanistan jana yalisimamisha shughuli za kibinadamu ikiwa ni, siku moja tu baada ya Taliban kuwazuia kuajiri wafanyakazi wanawake.

Taarifa ya pamoja ya taasisi za Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC), Save the Children na CARE International, ilisema kwamba mashirika yao hayawezi kufikia kwa ufanisi watoto, wanawake na wanaume walio na mahitaji makubwa nchini Afghanistan bila wafanyakazi wao wa kike.

Viongozi wa taasisi hizo wameonya kuwa, marufuku ya Taliban itaathiri utoaji wa msaada wa kuokoa maisha kwa mamilioni ya Waafghan na kuathiri maelfu ya kazi wakati hii ambapo mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaoikabili nchi hiyo maskini.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hatua ya serikali ya Taliban ya kusimamisha elimu ya chuo kikuu kwa wasichana wa Kiafghani iimekabiliwa na upinzani na ukosoaji mkali kitaifa na kimataifa.

Kutolewa kwa tangazo hilo kunaelezewa kama pigo jipya dhidi ya haki za wasichana na wanawake chini ya utawala wa Taliban nchini Afghanistan.

Kabla ya kuchukuliwa uamuzi huo, mtihani wa taifa wa kujiunga na vyuo vikuu ulikuwa umeshatangazwa na Wizara ya Elimu ya Juu kitaifa na katika mikoa, lakini uamuzi huo mpya wa Taliban wa kusimamisha masomo kwa wasichana katika vyuo vikuu na vituo vya mafunzo umezusha mkanganyo na sutafahamu katika mfumo wa elimu na masomo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *