China imesema mazungumzo ya kujaribu kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yapo katika hatua ya mwisho, na kusisitiza kwamba fursa ya kufufua mapatano hayo ya kimataifa ingalipo.
Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Chinaalisema hayo jana Jumatatu katika kikao na waandishi wa habari na kueleza kuwa, “Licha ya ugumu na changamoto zinazoyakabili mazungumzo (ya kuhuisha JCPOA), lakini kuna matumaini ya kufikia makubaliano.”
Ameeleza bayana kuwa, Beijing itaendeleza jitihada zake na kushirikiana na pande zote husika ili kuipatia ufumbuzi wa kidiplomasia na kisiasa kadhia ya nyuklia ya Iran, sambamba na kudumisha amani na uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati.
Jana Jumatatu pia, Msemaji Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema mlango wa Iran wa kufanya mazungumzo ya kuhusisha JCPOA upo wazi, na kwamba mapatano yanaweza kufikiwa iwapo nchi za Magharibi zitakuwa na irada njema ya kisiasa.
Nasser Kan’ani amesisitiza kuwa, mapatano ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yatafikiwa tu kwa kupatiwa ufumbuzi masuala yaliyosalia baina ya Jamhuri ya Kiislamu na pande nyingine za makubaliano hayo ya mwaka 2015, huku akikosoa mwenendo kinzani wa Marekani kwenye kadhia hiyo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitilia mkazo suala la kupewa dhamana kwamba Marekani haitajiondoa tena iwapo itaruhusiwa kurejea katika makubaliano ya JCPOA kama ilivyofanya mwaka 2018. Kadhalika Tehran inasisitiza kuwa haitafungamanisha maendeleo na ustawi wake na mazungumzo hayo ya kujaribu kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.