Ethiopia imetangaza kwamba imeanza tena safari za ndege kuelekea Mekele, makao makuu ya jimbo la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo huku huduma muhimu pia zikianza tena katika jimbo baada ya miaka miwili ya mapigano makali.
Huduma ambazo zimerejeshwa ni pamoja na usafiri wa anga, huduma za simu, misaada ya kibinadamu na huduma za benki baada ya vita vikali vya miaka miwili vilivyoua zaidi ya watu nusu milioni kama zinavyoonesha takwimu za Umoja wa Mataifa.
Safari za ndege zimeanza tena siku moja baada ya ujumbe wa serikali ya shirikisho ukiongozwa na spika wa bunge kutembelea mji wa Mekele na kufungua mlango wa kuboreshwa mawasiliano kati ya pande mbili zilizohusika katika vita hivyo vya miaka miwili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Ethiopia, Mesfin Tasew, amethibitisha habari ya kurejea safari za ndege za shirika hilo katika makao makuu ya jimbo la Tigray pamoja na kwamba mji huo unashikiliwa na waasi.
Amesema: “Tuko tayari kuwahudumia abiria wetu wanaosafiri kati ya Addis Ababa na Mekele na kutekeleza wajibu wetu wa kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi yetu.
Benki ya Biashara ya Ethiopia nayo imeanzisha upya huduma za kifedha katika baadhi ya miji ya jimbo la Tigray na kuruhusu wakazi wa miji hiyio kupata pesa taslimu baada ya serikali kufunga huduma hizo kwa muda wa mwaka mmoja.Mchambuzi mmoja wa masuala ya uchumi, Patrick Heinisch ameliambia Shirika la habari la Anadolu kwamba uchumi nchini Ethiopia umekuwa ukiimarika, ingawa polepole, tangu makubaliano rasmi ya amani yalipofikiwa na kukomesha vita, lakini kuna kazi kubwa lazima ifanyike ili kuwasaidia wananchi kurejesha walichopoteza wakati wa vita.