Afisa wa afya wa Yemen amesema takriban raia 3,000, wakiwemo wakimbizi wa Kiafrika, wamepoteza maisha au kujeruhiwa vibaya mwaka huu kutokana na mashambulizi ya mizinga na makombora ya vikosi vya jeshi la Saudi Arabia katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Sa’ada nchini Yemen.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Razih, Abdullah Musreeh, ameliambia shirika rasmi la habari la Yemen, Saba kwamba idadi ya wahanga wa kiraia katika mikoa ya Yemen inafikia 2,909, na kwamba idadi hiyo inahusu kipindi cha kati ya mapema Januari na mwishoni mwa Desemba mwaka huu.
Ameongeza kuwa watu wasiopungua 907 waliuawa au kujeruhiwa wakati wa mapatano ya usitishaji vita ya Umoja wa Mataifa yaliyodumu kwa miezi sita na kumalizika tarehe 2 Oktoba. Amesema watu hao walipoteza maisha katika mashambulizi ya wanajeshi vamizi wa Saudi Arabia.
Musreeh amesema hospitali yake ilipokea maiti 111 na majeruhi 796, wakiwemo waomba hifadhi wa Kiafrika, katika kipindi chote kilichotajwa, akisisitiza kuwa Saudi Arabia haijawahi kutekeleza mapatano ya usitishaji vita na vitendo vyake vya uhalifu vinaendelea bila kusitishwa.
Afisa huyo wa afya wa Yemen amebainisha kuwa wengi wa wale waliojeruhiwa vibaya walihamishiwa katika vituo vya matibabu katika mji mkuu Sana’a, kwani hospitali ya Razih ilikuwa na uhaba wa vifaa vya matibabu vya kutoa huduma muhimu.
Kando, Mkurugenzi wa Hospitali ya Monabbih Ali al-Ayashi amesema hospitali hiyo imepokea maiti 169 na majeruhi 1,833 tangu Januari.
Ameashiria kuwa utawala wa Riyadh unaendelea na jinai zake za kutisha dhidi ya taifa la Yemen na waomba hifadhi wa Kiafrika.
Ayashi pia amerejelea mbinu za kikatili za utesaji zinazofanywa na mamlaka za mpakani za Saudia dhidi ya raia wa Yemeni na wakimbizi wa Kiafrika, akisema kuwa vitendo hivyo vinakinzana na madai ya ufalme huo ya kuheshimu kanuni na mikataba ya kimataifa ya kibinadamu.
Saudi Arabia ilianzisha vita vikali dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 kwa ushirikiano na washirika wake wa Kiarabu na kwa msaada wa silaha na vifaa kutoka Marekani na mataifa mengine ya Magharibi.