Mfalme wa Jordan ameonya kuhusiana na hatua za utawala haramu za Israel za kushadidisha mivutano na jinai dhidi ya Wapalestina na kueleza kuwa, jinai hizo huenda zikapelekea kuibuka Intifadha mpya ya Wapalestina.
Mfalme Abdullah II wa Jordan amesema hayo katika mahojiano na televisheni ya CNN na kutahadharisha kuhusiana na hatari ya kushadidi hatua za uchochezi na kuzusha mivutano dhidi ya Wapalestina zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel.
Mfalme wa Jordan amesisitiza pia juu ya udharura wa kuheshimiwa hali ya kihistoria na kisheria iliyopo katika maeneo matukufu ya Kiislamu huko Beitul-Muqaddas na kukomesha aina yoyote ile ya uchochezi, hujuma na uvamizi.
Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqsa vimeongezeka mno.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo.
Mfalme wa Jordan kadhalika amesema nchi yake-ambayo ni khadimu na msimamizi wa Masjidul Aqsa- ipo tayari kwa ajili ya mgogoro na mivutano iwapo mistari yake myekundu juu ya eneo hilo takatifu lenye Kibla cha kwanza cha Waislamu itakiukwa.
Kuhusu kurejea madarakani Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, Mfalme wa Jordan amesema, “Iwapo kuna watu wanataka kuingia kwenye mzozo na sisi, tumejiandaa barabara. Tuna mistari yetu myekundi, na wale watakaojaribu kuikanyaga, tutakabiliana nao.”