Kampuni kubwa ya mafuta ya Marekani Exxon, ikiwa ni moja ya wauzaji wakubwa wa mafuta katika bara Ulaya, imushtaki Umoja wa Ulaya kwa kuyatoza makampuni ya mafuta ushuru mpya unaojulikana kama “kodi ya malipo kwa mapatano yanayopatikana bila kutoa jasho.”
Kodi hiyo mpya inatarajiwa kuanza kutekelezwa tarehe 31 Desemba na itakuwa sawa na asilimia isiyopungua 33 ya faida inayotozwa ushuru ya makampuni yote ya mafuta mwaka 2022 na 2023, ambayo ni asilimia 20 zaidi ya faida ya wastani iliyopatikana kati ya miaka ya 2018 hadi 2021.
Kampuni hiyo ya mafuta ya Marekani imesema Brussels imevuka mamlaka yake ya kisheria kwa kutoza ushuru ambao unatazamiwa kukusanya hadi euro bilioni 25. Exxon imesema imeushtaki Umoja wa Ulaya ili kuulazimisha kufuta kodi hiyo ya mapatano.
Mashtaka hayo yaliwasilishwa Jumatano na matawi ya shirika hilo yanayofanya kazi katika nchi za Ujerumani na Uholanzi, katika Mahakama Kuu ya Ulaya katika mji wa Luxembourg. Kesi hiyo ni hatua muhimu zaidi kuwahi kuchukuliwa katika sekta ya mafuta barani Ulaya baada ya serikali za bara hilo kuongeza ushuru dhidi ya mashirika ya mafuta kufuatia operesheni ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine. Kesi hiyo inatishia kusitisha ukusanyaji ushuru ambapo Tume ya Ulaya imetangaza kuwa inakusudia kukusanya euro bilioni 25 kwa ajili ya kusaidia kupunguza gharama ya nishati kwa raia wa nchi wanachama.
Inaonekana kuwa licha ya kuwepo matumaini ya kuimarika uhusiano wa pande mbili za bahari ya Atlantiki katika kipindi cha urais wa Joe Biden na kuanza kushirikiana tena Ulaya na Marekani katika nyanja tofauti, kwa mara nyingine tena tofauti kubwa imejitokeza kati ya pande hizo katika uga wa uchumi na biashara. Suala hilo bila shaka litapelekea kuongezeka hitilafu kati ya Brussels na Washington. Mara hii mjadala unahusu hatua ya Ulaya ya kufidia sehemu ya uharibifu uliosababishwa na ongezeko la bei ya mafuta na gharama za umeme na gesi kwa raia wa Ulaya, ambao umetokana na ushirikiano wa Ulaya na Marekani katika kutekeleza vikwazo vya pande zote dhidi ya Russia katika uwanja wa nishati.
Kwa kuifuata Marekani kibubusa na bila kuzingatia faida na madhara ya muda mrefu ya kukata ushirikiano wake na Russia, Ulaya iliamua kuweka vikwazo vikali dhidi ya Russia, jambo ambalo lilikabiliwa na radiamali kali ya Moscow ambayo iliamua kuupunguzia sehemu kubwa ya mauzo yake ya mafuta na gesi na hivyo kuisababishia Ulaya, ongezeko la mfumuko wa bei usio wa kawaida. Suala hilo limechochea mdororo mkubwa wa kiuchumi katika nchi nyingi za Ulaya, zikiwemo Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Sasa Umoja wa Ulaya unajaribu kuishirikisha Marekani ifidie ongezeko kubwa la gharama zinazotokana na sera na hatua za nchi za Magharibi dhidi ya Russia, kwa kuyatoza ushuru makampuni ya mafuta ya Marekani.
Tume ya Ulaya imesisitiza suala hilo kwa kusema: Kutozwa kodi mapato yanayopatikana bila kutotoa jasho kunaenda sambamba na sheria za Ulaya, na ushirikiano na mshikamano (kati ya sekta zinazozalisha na kutumia nishati) utahakikisha kwamba sekta nzima ya nishati inalipa sehemu yake ya gharama katika nyakati hizi ngumu.
Kwa upande wake, kampuni ya mafuta ya Exxon inadai kuwa pamoja na kwamba gharama kubwa ya nishati inatoa mashinikizo makubwa kwa familia na biashara za nchi za Umoja wa Ulaya, lakini kodi kubwa inayotozwa mapatano yanayopatikana bila ya kutoa jasho haifai na itawakatisha tamaa wawekezaji na kuwafanya wasiwekeze barani Ulaya na hatimaye kulifanya bara hilo liendelee kuagiza nishati kutoka nje.
Msemaji wa Exxon Casey Norton ameema: Exxon imetumia dola bilioni 3 kwa miradi ya kusafisha mafuta barani Ulaya katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, na imeongeza uzalishaji wake wakati huu ambapo Ulaya inajitahidi kupunguza uagizaji wa nishati kutoka Russia.
Pia, viongozi na maafisa wakuu wa Ulaya wameonya hivi karibuni kuhusu hatari ya kutokea vita vya kibiashara na Marekani kufuatia hatua ya Washington ya kupasisha sheria ya kuzuia ughali wa maisha mashuhuri kama IRA na kutishia kulalamikia Shirika la Biashara Duniani ikiwa Washington itaendelea kupuuza malalamiko ya Umoja wa Ulaya katika uwanja huo.
Ikulu ya White House inaisifu sheria ya IRA kama juhudi za kiubunifu za kufufua viwanda vya Marekani na kukuza teknolojia jadidika, lakini nchi za Umoja wa Ulaya zinaamini kuwa Marekani imeanzisha vita vya kibiashara na Ulaya kwa kutoa ruzuku kwa sekta yake ya uchumi wa kijani huku ikiyatoza ushuru makampuni ya Ulaya na hivyo kuyanyima fursa ya kushindana kwa usawa na makampuni ya Marekani.