Leo tarehe 30 Disemba ni siku ya kukumbuka ushiriki unaoshabihiana na ule wa Siku ya Ashura wa wananchi wa Iran wenye kuibua hamasa na watiifu kwa uongozi wa Faqihi Mtawala. Hamasa hiyo ilijiri Tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Disemba 2009, ambapo kulijiri tukio jingine katika historia iliyojaa fahari ya wananchi wa Iran ya Kiislamu.
Hamasa ya Tisa Dey ni nembo ya izza, uhuru, ung’amuzi au muono wa mbali wa wananchi wa Iran ambao walisimama wima kulinda misingi ya Uislamu na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu ambapo walitangaza kuwa iwapo adui ataonyesha uhasimu dhidi ya Uislamu basi watasimama kidete kukabiliana naye.
Katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, siku ya Tisa Dey hutajwa kuwa Yaumullah au Siku ya Mwenyezi Mungu na pia ni siku ya ung’amuzi au muono wa mbali.
Katika siku hii itakayobakia milele katika historia, taifa liliibua taswira nyingine katika anga ya Kiislamu ya Iran na kuwafanya maadui wa Mwenyezi Mungu na dini yake kukata tamaa na kujaza furaha katika moyo wa Imam wa Zama (AS) na Naibu Wake halali Ayatullah Khamenei (Allah Ambariki).
Inaweza kusemwa kwamba siku ya Tisa Dey ni siku ya ushindi wa jeshi la Mwenyezi Mungu juu ya jeshi la Shetani. Ni siku ya ghadhabu za wananchi wa Iran na kuteremshwa hasira zao tukufu dhidi ya baadhi ya watu wazembe na mamluki ambao walivunjia heshima siku ya Ashura ya Imam Hussein (AS).
Siku hii, watu wa Iran waliwaangamiza viongozi wa fitna na kwa msingi huo tarehe 9 Dey uhalali wa kisiasa wa mfumo wa Kiislamu wa Iran kwa mara nyingine tena ulitangazwa kwa walimwengu kwa mahudhurio ya makumi ya mamilioni ya watu mjini Tehran na miji mingine ya Iran ya Kiislamu.
Siku ya 9 Dey 1388 Hijria Shamsia sawa na Desemba 30, 2009 ni ukumbusho wa matembezi ya mamilioni ya watu wa Iran katika kutangaza kuwapinga waasi waliofuata njia mbaya kwa kisingizio kisicho na msingi cha eti kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa muhula wa10 wa rais wa Iran.
Kwa mnasaba wa kukumbuka siku hii ya kihistoria, jana mamilioni ya wananchi wa Iran walishirki katika matembezi na kutangaza tena utiifu wao kwa mfumo wa Kiislamu. Matembezi hayo pia yamefanyika kwa mnasaba wa mwaka wa tatu wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Hajj Qassem Soleimani.
Washiriki wa matembezi hayo wametoa taarifa na kusema adui ameshindwa katika mradi wake wa hivi karibuni wa kuibua ghasia za mtaani lakini wamesisitiza kuwa fitina za adui zingali zinaendelea. Aidha taarifa hiyo imesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mbeba bendera ya ustaarabu mpya wa Kiislamu na mabadiliko mapya katika mfumo wa utawala duniani.