Idadi ya vifo katika mkasa wa mlipuko wa lori la kubeba gesi Afrika Kusini yafikia 34

Wizara ya Afya ya Afrika Kusini imetangaza kuwa, idadi ya watu walioaga dunia katika mlipuko wa lori la kubeba gesi uliotokea Jumamosi iliyopita jirani na mji wa Johannesburg imeongezeka na kufikia wahanga 34.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya Afrika Kusini imeeleza kuwa, miongoni mwa walioaga dunia wamo wapita njia ambao walikuwa karibu na tukio hilo masafa machache kabla ya lori hilo lililokuwa limebeba gesi kulipuka.

Aidha wafanyakazi 11 wa sekta ya afya wa hospitali moja iliyo jirani na lilipotokea tukio hilo ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha yao katika mmkasa huo wa kusikitisha.

Duru kutoka nchini Afrika Kusini zinasema kuwa, lori hilo la kubeba gesi lilikwama chini ya daraja moja karibu na hospitali, lakini pia kwenye makaazi ya watu Jumamosi asubuhi juma lililopita huko Boksburg, yapata kilomita 40 mashariki mwa mji wa Johannesburg.

Taarifa zaidi ziinasema kuwa, “wazima moto waliingilia kati, lakini kwa bahati mbaya lori hilo lililipuka,” hayo ni kwa mujibu wa William Ntladi, msemaji wa idara ya huduma za dharura katika eneo hilo.

Afisa mmoja amesema kuwa, uchunguzi umeanza ili kufahamu sababu za lori hilo kulipuka. “Lazima kuweko na uchunguzi wa kina kuhusu jinsi lori linalobeba LP Gas linaweza kwenda chini ya daraja la kiwango cha chini. Kwa kawaida malori haya hayaruhusiwi kufanya hivyo,” amebainisha afisa huyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *