Kiongozi wa Korea Kaskazini ametoa amri ya kuzalishwa makombora mapya ya balestiki ya kuvuka mabara, sambamba na kuongezwa kiwango cha silaha za nyuklia za ‘kimkakati’ kwa ajili ya kukabiliana na tishio la Marekani.
Kim Jong-un amenukuliwa akisema hayo leo Jumapili na shirika rasmi la habari la nchi hiyo KCNA baada ya kumalizika mkutano muhimu chama tawala cha Wafanyakazi mjini Pyongyang na kusisitiza kuwa, Korea Kaskazini inapaswa kuwa tayari na kujiandaa kwa makabiliano na Marekani.
Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amelitaka jeshi la nchi hiyo kujiimarisha na kujiweka tayari kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vyovyote vya maadui wa nchi hiyo ya Peninsula ya Korea.
Kim amesema agizo lake la kutaka kuongezwa kiwango cha silaha za nyuklia za nchi hiyo sambamba na kuzalishwa makombora mapya ya balestiki ya kuvuka mabara linakusudia kulilinda taifa hilo mkabala wa vitisho vya Marekani na Korea Kusini.
Kim Jong-un ameeleza bayana kuwa, Korea Kaskazini itatumia nguvu zote kudumisha amani na kulinda uhuru na mamlaka yake ya kujitawala. Amesema, “Pyongyang inapaswa kujiweka tayari barabara hususan kwa makabiliano, kwa shabaha ya kulinda hadhi ya taifa letu.”
Wakati huohuo, jeshi la Korea Kaskazini limefyatua kombora lake la balestiki la masafa mafupi kuelekea upande wa Japan mapema leo Jumapili.
Majeshi ya Japan na Korea Kusini yamethibitisha habari ya Pyongyang kuvurumisha kombora lake la balestiki la masafa mafupi, lililotua katika eneo la Bahari ya Mashariki, linalofahamika kwa jina jingine kama Bahari ya Japan.