IMF: 2023 utakuwa mwaka mgumu kwa uchumi wa dunia

Mkuu wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF ametangaza kuwa thuluthi moja ya uchumi wa dunia itakabiliwa na mdororo wa kiuchumi mwaka 2023.

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa ulitangaza Oktoba 2022 kwamba ukuaji wa uchumi wa dunia utapungua katika mwaka 2023.
Vita nchini Ukraine, mashinikizo ya mfumuko wa bei na viwango vya juu vya riba vilivyopangwa na benki kuu kama vile Hifadhi ya serikali kuu ya Marekani kwa lengo la kupunguza shinikizo la bei vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia kuzorota kwa ukuaji wa uchumi duniani.
Mkuu wa IMF Kristalina Georgieva, alitangaza jana kuwa “2023 utakuwa mwaka mgumu zaidi kuliko mwaka tuliopita, kwa sababu uchumi wa Marekani, Umoja wa Ulaya na China ambazo zote tatu ndizo nguvu kuu za kiuchumi duniani utashuka kwa wakati mmoja”.
Bi Georgieva ameongeza kuwa, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimepata madhara makubwa kutokana na vita kati ya Russia na Ukraine, na nusu ya nchi hizo zitakumbwa na mdororo wa uchumi katika mwaka mpya.
Mkuu huyo wa IMF ambaye hivi majuzi alisafiri hadi China kuzungumzia shirika hilo la fedha la kimataifa, ameongeza kuwa: kufikia kiwango cha juu zaidi mripuko wa Corona katika miezi ijayo huenda kukaathiri uchumi wa nchi hiyo katika mwaka huu na kuchelewesha ukuaji wa uchumi kikanda na kimataifa.
Mkuu wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa ametahadharisha kwamba ukuaji hasi wa uchumi wa China utakuwa na athari mbaya kwa eneo na kwa ukuaji wa uchumi kimataifa.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *