9 wafariki, wakiwemo watoto 6 katika msongamano wa mkesha wa mwaka mpya Uganda

Watu wasiopungua tisa wamefariki dunia wakiwemo vijana wadogo sita katika msongamano uliotokea wakati wa sherehe za mkesha wa mwaka mpya katika duka kuu moja la mji mkuu wa Uganda, Kampala.

Kwa mujibu wa msemaji msaidizi wa polisi ya Uganda Luke Owoyesigyire, inasemekana tukio hilo lilitokea usiku wa manane wa kuamkia jana katika duka kuu la Freedom City jijini Kampala baada ya mshereheshaji wa hafla hiyo kuwahimiza waliohudhuria kutoka nje ili kwenda kuangalia maonyesho ya fataki na fashfashi na kwamba baada ya onyesho hilo kumalizika, ukazuka mkanyagano uliosababisha vifo vya papo hapo vya watu watano.

Owoyesigyire ameongeza kuwa watoaji huduma za dharura waliwakimbiza majeruhi kadhaa hadi hospitalini na kwamba baadaye jumla ya vifo tisa vilithibitishwa kufuatia msongamano huo wa watu.

Taarifa zinasema, idadi ya vifo vya mkasa huo inaweza kuongezeka.

Wakati huouo, maafisa wa upelelezi wa Polisi wamesema, wanamsaka muandaaji wa hafla hiyo aitwaye Abbey Musinguzi ambaye inasemakana kuwa amejificha.

Aidha kutokana na kuripotiwa idadi kubwa ya vijana wadogo waliofariki katika tukio hilo, polisi imesema inafuatilia pia suala hilo kwa kuzingatia kwamba vigezo vya umri vilivyowekwa kwa ajili ya kuhudhuria hafla za usiku, watoto walio na umri hadi miaka 18 hawatakiwi kuhudhuria tukio lolote la burudani baada ya saa kumi na moja jioni

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *