Malawi siku ya Jumatatu imeahirisha kufunguliwa kwa shule za msingi na sekondari kwa angalau wiki mbili kutokana na mlipuko wa kipindupindu.
Muhula huo mpya ulipangwa kuanza Januari 3, lakini ongezeko la visa vya maambukizi ya kipindupindu na vifo vimeilazimu serikali kufuta mipango ya kufungua shule inapokabiliana na mlipuko huo.
Hatua hiyo, kulingana na serikali, inahusu miji ya Blantyre na Lilongwe.
Jopo kazi la rais wa nchi hiyo kuhusu corona na kipindupindu limesema katika taarifa kwamba wanafunzi wengine wote katika wilaya zote za afya, mamlaka husika zinapaswa kuimarisha uzingatiaji wa hatua zilizopendekezwa za kudhibiti kipindupindu, ikiwa ni pamoja na chanjo ya kipindupindu kwa wale ambao bado hawajachanjwa.
Katika sasisho lake la hivi punde lililotolewa Desemba 22, serikali ilisema kuwa kipindupindu kimeua watu 410 nchini Malawi tangu Februari 2022, huku 13,837 wakiwa wamepimwa ugonjwa huo kati yao 338 wakilazwa hospitalini.
Kipindupindu ni ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na kula chakula au kunywa maji yaliyo na bakteria aina ya Vibrio cholera, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema.
Kipindi cha kuibuka dalili za maradhi hayo ni kati ya saa 12 na siku tano baada ya kula chakula au kunywa maji machafu. Ugonjwa huo unasalia kuwa tishio la kimataifa kwa afya ya umma, lakini ni ugonjwa unaotibika.
Mwezi Novemba, Malawi ilipokea dozi milioni 2.9 za chanjo ya kipindupindu kutoka kwa Umoja wa Mataifa wakati mlipuko huo ulipokuwa ukienea.
Malawi, ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi barani Afrika, ina wakazi milioni 18 na wengi wao wanategemea kilimo cha kujikimu. Hata hivyo, hali ya usalama wa chakula ni mbaya kwa sababu ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa.