Makumi ya Wamarekani, wahanga wa umaskini na baridi kali, huku mabilioni ya dola yakitumiwa kwenye vita vya Ukraine

Wakati mji wa Buffalo ulioko katika jimbo la New York kaskazini-mashariki mwa Marekani, ukihangaika kujikwamua kwenye athari mbaya za theluji na dhoruba kali, matatizo yaliyosababishwa na maafa hayo makubwa yamedhihirisha zaidi ukosefu wa usawa wa kiuchumi na ubaguzi wa kimbari katika mji huo na Marekani kwa ujumla.

Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa, kukata tamaa na kufadhaika kwa wananchi ambao wamekwama katika nyumba zilizoganda kwa siku kadhaa, ukosefu wa chakula na mitaa ambayo bado imefunikwa na theluji, vimezidisha mapengo makubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo yameugawa mji huo kwa muda mrefu. Maafisa wa serikali katika mji wa Buffalo wamesema zaidi ya maiti 30 zimepatikana katika nyumba, magari au chini ya theluji. Mkazi mmoja wa Buffalo amesema katika mahojiano na gazeti la Washington Post kwamba: “Jiji hili limeathiriwa sana na matatizo ya kimuundo. Mashaka mengi yamezipata familia za watu maskini na wasio wazungu.” Buffalo, ambayo inatambuliwa kuwa mojawapo ya miji maskini zaidi nchini Marekani, bado inasumbuliwa na hali ya ubaguzi wa rangi. Kulingana na ripoti ya Washington Post, mji huo pia mwaka huu umeathiriwa na janga la Corona.

Umaskini mkubwa na vifo vya makumi ya Wamarekani katika mji wa Buffalo, vimeripotiwa huku serikali ya Marekani ikitoa msaada wa dola bilioni 40 kwa Ukraine katika bajeti ya mwaka huu 2023 ya nchi hiyo. Bajeti hiyo inajumuisha misaada ya kifedha, kijeshi na silaha kwa serikali ya Kyiv. Mnamo 2022, utawala wa Joe Biden uliipatia Ukraine jumla ya dola bilioni 40 kama msaada wa kifedha na silaha. Kwa njia hii, msaada wa kifedha, kijeshi na silaha wenye thamani ya dola bilioni 80 wa Marekani kwa Ukraine umetolewa kwa ajili ya kuendeleza vita nchini Ukraine huku makumi ya raia wa Marekani wakifariki dunia au kupata madhara makubwa kutokana na umaskini katika mji wa Buffalo ulioathjiriwa na theluji na baridi kali. Vilevile, bajeti ya kijeshi ya dola bilioni 858 kwa 2023 imepitishwa huko Marekani wakati ilikuwa ikitarajiwa kwamba, kiwango kikubwa cha pesa kingetumika katika kuboresha hali ya kijamii, huduma mbaya za afya na miundombinu iliyochakaa ya nchi hiyo. Aidha kwa kutilia maanani ahadi za chama cha Democrats na Rais Joe Biden, bajeti ya kijeshi ya Marekani inapaswa kuwa na mwelekeo wa kushuka na kupunguzwa. Hivyo, kwa kuzingatia mahitaji ya haraka ya ndani ya Marekani, suala hili kwa hakika lina maana ya kuwanyima watu wa nchi hiyo mahitaji mengi muhimu hususan tabaka za watu wenye uhitaji. Inatupasa pia kusema hapa kuwa, badala ya kutenga rasilimali muhimu za kifedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu, haswa barabara, madaraja, mitambo ya maji na umeme kupitia njia ya kupunguza bajeti ya jeshi, serikali ya shirikisho ya Marekani imekuwa ikiongeza bajeti ya jeshi la nchi hiyo kila mwaka kwa mujibu wa maslahi ya duru za kijeshi na wamiliki wa viwanda.

Msaada wa makumi ya mabilioni ya dola wa Washington kwa Ukraine unatolewa kwa malengo ya sera ya nje ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kudhoofika uwezo wa kijeshi na kiuchumi wa Russia kama mmoja wa washindani wa kimataifa wa Marekani. Vilevile wakandarasi wa masuala ya ulinzi wa Marekani wameripotiwa kuwa na maslahi makubwa katika vita vya Ukraine.

Kwa sasa utawala wa Biden umetoa maagizo kwa makampuni ya silaha kujaza hifadhi ya silaha za Marekani, ambayo imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na usafirishaji zana za kijeshi kwenda Ukraine. Makampuni haya yana ushawishi mkubwa katika Bunge la Kongresi na wakati huo huo yana satua kubwa katika Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon. Vilevile tangu mwisho wa Februari 2022 wakati vita vya Ukraine vilipoanza, Washington imewalazimisha na kuwahimiza washirika wake wa Magharibi, hasa wa Ulaya, kutuma aina mbalimbali za zana za kijeshi na silaha nchini Ukraine. Suala hili limepelekea kupungua kwa kiasi kikubwa kwa hifadhi ya silaha na zana za kivita katika nchi hizo. Wakati huo huo, kuongezeka hofu na woga wa nchi hizo kwa Russia kumezidisha maombi ya nchi za Ulaya wanachama wa NATO na zisizo wanachama ya kununua silaha zaidi kutoka Marekani. Mwaka 2021 serikali ya Marekani iliidhinisha mauzo 14 makubwa ya silaha kwa wanachama wa NATO, ambayo yalikuwa na thamani ya jumla ya dola bilioni 15.5.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *