Hisia na misimamo ya nchi za Kiarabu kwa uamuzi wa serikali ya Netanyahu wa kupanua vitongoji haramu vya wazayuni

Kufuatia uamuzi uliotangazwa na waziri mkuu mpya wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba serikali yake itaendeleza ujenzi haramu wa vitongoji, baadhi ya nchi za Kiarabu zimelaani uamuzi huo na kuipa indhari Tel Aviv kuhusiana na madhara ya hatua hiyo.

Katika kikao cha bunge la utawala haramu wa Israel cha kulipigia baraza lake jipya la mawaziri kura ya kuwa na imani nalo, Netanyahu alitangaza kuwa, kuendeleza ujenzi wa vitongoji ni moja ya vipaumbele muhimu sana vya serikali yake. Ujenzi wa vitongoji ni moja ya jinai kuu ambazo utawala wa Kizayuni unawatendea Wapalestina. Jinai hiyo inatekelezwa kufanikisha malengo ya uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu ya utawala huo; na imepelekea kunyakuliwa ardhi, kuporwa nyumba na makazi ya Wapalestina na kuwafanya wananchi hao madhulumu waishi maisha ya ukimbizi.

Ukweli ni kwamba, kwa kuendeleza ujenzi wa vitongoji, utawala wa Kizayuni umejaribu, kwa upande mmoja, kutatua tatizo lake la kutokuwa na eneo la kijiografia; na kwa upande mwingine, na tangu ilipoanza karne hii ya 21, kufanya kila njia ili kuhakikisha inakamilisha mkakati wa kuihodhi na kuikalia kwa mabavu ardhi yote ya Palestina.

Taathira hasi za kijamii na kiusalama za ujenzi wa vitongoji zimekuwa na madhara makubwa kwa Wapalestina, mpaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likaamua katika azimio 2334 lililopitisha mwaka 2016 kulaani jinai hiyo ya utawala ghasibu wa Israel; lakini serikali ya wakati huo ya utawala huo haramu iliyokuwa ikiongozwa na Netanyahu ililipuuza azimio hilo kutokana na uungaji mkono iliokuwa ikipata kwa aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo Donald Trump.

Hivi sasa, na huku Netanyahu akisisitizia tena suala la kuongeza idadi ya vitongoji, na zikiwa zimepita siku tano tu tangu serikali yake iingie madarakani, unashuhudiwa ukatili na ukandamizaji mkubwa dhidi ya Wapalestina. Sisitizo hilo la waziri mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni na kushadidi ukandamizaji dhidi ya Wapalestina vimeibua sauti za malalamiko za baadhi ya nchi za Kiarabu.

Bunge la Qatar limelaani mpango wa baraza la mawaziri la utawala haramu wa Israel wa kutaka kupanua ujenzi haramu wa vitongoji na kutahadharisha juu ya madhara ya hatua hiyo. Aidha limeyataka mabunge yote ya nchi za Kiarabu yachukue hatua ya pamoja katika kulaani jinai hiyo. Nalo bunge la Waarabu limetoa taarifa, ambayo imelaani uamuzi na hatua ya baraza jipya la mawaziri la Tel Aviv dhidi ya Wapalestina. Kabla ya taarifa hiyo, bunge la mashauriano la Oman, lilipiga marufuku kuanzisha mahusiano ya aina yoyote na utawala huo unaoikalia Quds kwa mabavu.

Hatua hizi za mabunge ya Kiarabu zinaonyesha kuwa, kinyume na hatua ya nchi chache za Kiarabu zinazoshupalia kustawisha uhusiano na Israel na kuliweka pembeni suala la Palestina, mabunge kadhaa ya nchi za Kiarabu yameamua kuungana na fikra za waliowengi na wananchi wa Ulimwengu wa Kiarabu kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa Wapalestina. Mshikamano huo wa kisiasa katika kuwaunga mkono Wapalestina unaweza kuongeza mashinikizo dhidi ya utawala dhalimu wa Kizayuni.

Sambamba na uungaji mkono huo wa mabunge na wananchi wa mataifa Kiarabu, kuna nia ya dhati na azma thabiti pia ya makundi ya mapambano ya Palestina ya kukabiliana na utawala haramu wa Kizayuni. Sio tu makundi hayo hayajatishika kwa vitisho vilivyotolewa na serikali mpya na yenye misimamo mikali ya kifashisti ya utawala wa Kizayuni, lakini pia yamejiweka tayari kikamilifu kukabiliana na ukatili wa utawala huo dhalimu. Kuhusiana na suala hilo, makundi ya Muqawama ya Palestina yameshatoa indhari pia kwa utawala ghasibu wa Israel juu ya matokeo mabaya ya hatua na maamuzi yake.

Nukta muhimu hapa ni kwamba, mshindwa wa mchakato huu ni baadhi ya nchi ikiwemo Saudi Arabia ambazo zinafuata mkondo wa kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel pasi na kutilia maanani harakati na vuguvugu la wananchi wa Ulimwengu wa Kiarabu. Harakati hiyo inayofuata njia kinyume na mkondo mkuu wa matukio ya ukanda huu kuhusiana na Palestina, inaweza kuuletea matokeo mengi mabaya na yenye madhara utawala wa Aal Saud.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *