Putin atuma manowari yenye makombora ya hypersonic Bahari ya Atlantic, Hindi

Rais Vladimir Putin wa Russia ameagiza kutumwa katika Bahari ya Atlantic na Bahari Hindi meli ya kivita iliyosheheni makombora ya hypersonic huku vita vya Ukraine vikipamba moto.

Rais Putin jana Jumatano kupitia njia ya video, alishiriki katika hafla ya kuiaga manowari hiyo ya kijeshi ya ‘Admeli Gorshkov’ kuelekea Bahari ya Atlantic na Bahari Hindi. Sergei Shoigu, Waziri wa Ulinzi wa Russia na Igor Krokhmal, Kamanda wa manowari hiyo walishiriki pia hafla hiyo.

Kabla ya kuagiza kuondoka kwa meli hiyo ya kijeshi, Rais Putin amesema, “Meli hii imesheheni mfumo wa kisasa wa makombora ya hypersonic wa Zircon. Naitakia kheri timu (ya wanajeshi wa baharini) na nawatakia ufanisi katika huduma yao kwa maslahi ya ardhi yetu.”

Mwishoni mwa Disemba pia, Russia ilipeleka manowari tatu za kubebea makombora katika Bahari Nyeusi na kuziweka meli hizo za kivita katika hali ya tahadhari. Manowari hizo za kijeshi zimesheheni makombora 20 aina ya Kalibr. Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Russia,  Sergei Shoigu, kombora moja la Kalibr linaweza kubeba kichwa cha nyuklia chenye uzani wa kilo 500.

Katika hotuba yake ya kufunga mwaka wa 2022, Rais wa Russia, Vladimir Putin alisisitiza kuwa, Moscow haitaziruhusu nchi za Magharibi kuwatumia watu wa Ukraine kwa ajili ya kuigawa na kuidhoofisha Russia.

Haya yanajiri siku chache baada ya Marekani kutangaza kuiongezea Ukraine msaada wa kijeshi wa dola bilioni 1.85 ikiwa ni pamoja na kuipelekea Ukraine mfumo wa makombora wa Patriot.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *