Mpalestina aliyeshikiliwa kwenye gereza la Israel kwa muda mrefu zaidi wa miaka 40 aachiwa huru

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umemwachilia huru mateka Mpalestina aliyeshikiliwa kwenye gereza la utawala huo dhalimu kwa muda mrefu zaidi wa miaka 40.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Al-Mayadin, Karim Younes, mateka Mpalestina mwenye umri wa miaka 66 ameachiwa huru baada ya kushikiliwa kwa muda wa miaka 40 katika jela za utawala haramu wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa Al-Mayadin, Karim Younes, aliachiliwa huru ghafla na bila ya kupewa taarifa kabla, alfajiri ya Alkhamisi.
Wizara ya Masuala ya Mateka na Wafungwa Wapalestina imetangaza kuwa, utawala ghasibu wa Kizayuni ulipanga kumwachilia huru Mpalestina huyo mapema jana asubuhi katika eneo la Raanana katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na mbali na makazi ya familia yake katika kitongoji cha Ara, ili kuzuia kufanyika hafla au sherehe ya kumlaki na kumkaribisha Mpalestina huyo aliyeshikiliwa kwa muda mrefu zaidi katika jela za utawala huo.
Hata hivyo kinyume na hatua ulizochukua utawala haramu wa Israel na vitisho ulivyotoa vya kupiga marufuku kufanyika sherehe ya kuachiliwa huru Karim Younes, mara baada ya kupata taarifa za kuachiwa huru kwake kutoka jela ya Hadarim, familia ya mateka huyo na idadi kubwa ya wanaharakati na wananchi wa kawaida wa Palestina, walielekea mahali alipokuwapo katika kitongoji cha Ara.

Baada ya kuachiwa huru, Karim Younes aliwaambia waandishi wa habari: “Ningependa ninyakue uhuru wangu nikiwa pamoja na ndugu zangu wengine walioko gerezani… lakini natumai baada ya muda si mrefu, tutaweza kusherehekea kuwa huru kwa mateka wote”.
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulimkamata Karim Younes tarehe 6 Januari 1983 na kumhukumu kifungo cha maisha jela.

Ili kufikia malengo yake ya kujipanua, utawala haramu wa Israel kila siku hushambulia maeneo tofauti ya Palestina na kuwaua shahidi, kuwajeruhi au kuwakamata na kuwatia jela wananchi madhulumu wa Palestina.

Kuna mateka wa Kipalestina wapatao 4,700 wanaoshikiliwa kwa sasa katika magereza ya Israel, wakiwemo watoto 150 na watu 835 wanaoshikiliwa bila kuwa na kesi wala kufunguliwa mashtaka.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *