Indhari baada ya kuongezeka joto, katikati ya msimu wa baridi barani Ulaya

Mamia ya vituo vya hali ya hewa kote Ulaya vimerekodi viwango vya juu vya joto kila siku kuwahi kufikiwa katika miezi ya Desemba au Januari. Huduma kadhaa za kitaifa za hali ya hewa na maji kutoka bara hilo zinathibitisha kuwa mwaka wa 2022 ulikuwa wa joto zaidi katika historia katika nchi hizo.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambalo limeonya kuwa yamkini hali ikaendelea kuwa mbaya zaidi katika siku za usoni. Shirika hilo limebaini kuwa halijoto iliyozidi nyuzijoto 20 za selisiasi ilitokea katika nchi nyingi za bara hilo hata Ulaya ya Kati na kwamba katika mataifa kadhaa, kutoka Uhispania hadi Ulaya Mashariki, rekodi zingine za halijoto ya kitaifa zilivunjwa na maeneo mengi katika miezi ya Desemba na Januari.

Kwa mfano  zaidi ya halijoto ya juu katika siku ya mwisho ya mwaka 2022 ilikuwa nyuzijoto 18.9°C iliyofikiwa Warsaw, mji mkuu wa Poland, ambayo ilipita nyuzijoto 13.8°C zilizorekodiwa mwezi Januari mwaka 1993.

Mzunguko na ukubwa wa matukio ya joto kali, ikiwa ni pamoja na mawimbi ya joto baharini, umeongezeka katika miongo ya hivi karibuni na unakadiriwa kuendelea kuongezeka. Ongezeko la joto duniani linatokana na uchafuzi wa mazingira hasa kupitia gesi chafuzi za viwanda na magari. Umoja wa Mataifa umeitisha mikutano kadhaa ya kimataifa kwa ajili ya kuhimiza walimwengu kulinda mazingira. Nchi za Afrika ambazo zina mchango mdogo zaidi katika uchafuzi wa mazingira ndizo zilizoathirika zaidi kwani zimekuwa zikishuhudia majanga mengi ya kimaumbile kama vile ukame, mafuriko na ongezeko la kina cha bahari.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *