Kurudi nyuma kwa serikali ya Macron dhidi ya upinzani

Serikali ya Ufaransa Jumanne wiki hii ilidokeza uwezekano wa kutazamwa umpya mpango tata wa Rais Emmanuel Macron wa kubadilisha sheria za pensheni. Hatua hiyo inaonekana kuwa ni kusalimu amri mbele ya wapinzani wa mpango huo.

Waziri Mkuu wa Ufaransa, Élisabeth Borne amesema kabla ya mazungumzo na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi, ambao wanapinga vikali mabadiliko hayo, kwamba suala la kuainishwa umri wa kustaafu wa miaka 65 linawezi kubadilika na kwamba kunaweza kuwa na njia nyingine za kuisaidia serikali kufikia malengo yake ya kujenga mlingano katika mfumo wa pensheni hadi kufikia 2030. Élisabeth Borne amesema mpango huu, ambao unatambuliwa kuwa sehemu muhimu zaidi ya sera ya ndani ya Macron katika muhula wake wa pili wa uongozi, utawasilishwa katika mkutano wa baraza la mawaziri Januari 23 na katika Bunge la Ufaransa Februari 1. Maelezo kamili ya mpango huu, ambao sehemu yake kuu, yaani ongezeko la umri wa kustaafu kutoka umri wa miaka 62 ya sasa hadi miaka 65, imekabiliwa na upinzani kamili wa vyama vya biashara na wafanyakazi vya Ufaransa, yatatangazwa Mnamo Januari 10. Marekebisho haya ya kimsingi yaliyopendekezwa na Macron ndio mpango mpana zaidi katika mlolongo wa mageuzi ya miongo kadhaa ya serikali za mrengo wa kushoto na mrengo wa kulia za Ufaransa katika sheria ya pensheni ili kukomesha nakisi ya bajeti ya nchi hiyo.

Katika hotuba yake iliyotoa mwanzo wa mwaka mpya, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, alisema katika ujumbe wenye utata kuhusu mfumo wa pensheni ambao ulisababisha harakati za Vizibao vya Njano tangu Novemba 2018, kwamba mageuzi haya ya pensheni yatatekelezwa mwaka huu wa 2023. Kurekebisha mfumo wa pensheni ilikuwa miongoni mwa ahadi kuu za Macron katika uchaguzi wa rais wa 2017, lakini mapendekezo yake ya awali katika suala hili yalichochea maandamano na migomo nchini Ufaransa. Maandamano na migomo hiyo, ambayo ilijulikana kama maandamano ya Vizibao vya Njano, yamechochea mgogoro mkubwa na taharuki ya miezi kadhaa nchini Ufaransa.

Kurudi nyuma kwa serikali ya Macron dhidi ya matakwa ya upinzani, ikiwa ni pamoja na vyama vya wafanyikazi vinavyopinga kuongezwa umri wa kustaafu, kumetokana na ongezeko la wimbi la upinzani katika jamii ya Ufaransa, haswa migomo iliyoenea nchini humo ya wafanyabiashara na sekta mbalimbali. Kwa hakika, Emmanuel Macron anajua vyema kwamba hana uwezo wa kukabiliana na wapinzani wa sera zake, kwa msingi huo, ameamua kulegeza kamba na kuweka kando mpango wake wa awali walau kwa wakati huu, akijaribu kunyamazisha sehemu kubwa ya upinzani.

Kwa ujumla ni kwamba, hatua za Macron zimesababisha hisia hasi katika jamii ya Ufaransa, ambayo inailaumu serikali kwa kutekeleza sera na kuchukua hatua dhidi ya Urusi na matokeo yake mabaya, ambayo ni pamoja na uhaba mkubwa wa gesi, ongezeko kubwa la mfumuko wa bei, na mdororo wa kiuchumi unaoinyemelea nchi hiyo. Wakati huo huo, ongezeko kubwa la mfumuko wa bei na gharama ya maisha nchini Ufaransa na kutokuwapo mlingano baina ya gharama za matumizi na mapato ya sehemu kubwa ya Wafaransa, kumesababisha wimbi la migomo zaidi katika nchi hiyo ya Ulaya.

Kwa mfano tu, hospitali kadhaa kubwa kwa sasa zinasumbuliwa na hali mgumu sana baada ya madaktari wake wengi, kuanza mgomo unaoendelea hadi tarehe 8 mwezi huu wa Januari wakidai nyongeza ya mishahara. Madaktari na madaktari bingwa wa hospitali binafsi nchini Ufaransa wamekuwa kwenye mgomo tangu mwanzoni mwa Januari 2023 na wanadai kupewa mshahara mara mbili ya mshahara wao wa sasa. Kufuatia mgomo huo, asilimia 80 ya ofisi za madaktari kote Ufaransa zilifungwa. Mmoja wa hao ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba: “Migomo sio kawaida katika taaluma yetu. Ikiwa tumefikia hatua hii, ni kwa sababu hatuna njia nyingine ya kuwasilisha sauti yetu.”

Baada ya mgomo wa kitaifa wa madaktari wa Ufaransa mapema Disemba 2022, huu ni mgomo wa pili ya sekta hiyo katika mwezi mmoja uliopita kwenye nchi hiyo ya Ulaya Magharibi. Kabla ya hapo, Ufaransa ilikumbwa na mgomo mkubwa wa makampuni ya nishati katika uwanja wa uzalishaji na usambazaji wa mafuta, ambao ilisababisha matatizo mengi kwa serikali ya Paris.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *