‘Uhuru wa kujieleza’, kisingizio cha kukaririwa cha Charlie Hebdo kwa ajili ya kutusi matukufu wa kidini

Jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo, ambalo huko nyuma lilidhalilisha na kumvunjia heshima mara kadhaa Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw), sasa limeimarisha chuki zake dhidi ya dini hii tukufu kwa kutukana na kuwavunjia heshima viongozi wa kidini na kisiasa wa Kiislamu.

Jarida la dhihaka la Charlie Hebdo hivi karibuni liliandaa shindano la kimataifa la uchoraji kwa lengo la kuchapisha vikatuni vya kutusi na kuwavunjia heshima viongozi wa kidini na kisiasa wa Iran, jambo ambalo liliamsha hasira na ukosoaji mkali dhidi ya jarida hilo pamoja na siasa za chuki za serikali ya Ufaransa dhidi ya Uislamu kwa kisingizio eti cha kutetea uhuru wa kujieleza. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilimwita balozi wa Ufaransa mjini Tehran, Nicolas Roche, na kumtaka awafikishie viongozi wa Paris malalamiko ya Tehran kuhusu kitendo hicho cha matusi.

Catherine Colonna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, alitoa matamshi yasiyo ya kimantiki kufuatia malalamiko ya Iran kwa kitendo hicho cha matusi kwa kusema: “Usisahau kuwa nchini Ufaransa, tofauti na ilivyo huko Iran, kuna uhuru wa kujieleza ambao unasimamiwa na jaji ndani ya mfumo wa mahakama huru, suala ambalo bila shaka Iran hailijui vizuri.”

Ufaransa, sawa na nchi nyingine za Magharibi, siku zote imekuwa ikitumia kisingizio cha uhuru wa kusema kuhalalisha vitendo vya udhalilishaji na matusi dhidi ya Waislamu, wanazuoni, viongozi na maeneo yao matakatifu, katika hali ambayo sharti la uhuru wa kuzjieleza ni kuepuka kuwatukana watu wengine na maeneo yao matakatifu. Kwa mujibu wa Hati ya Sheria za Kimataifa, ni marufuku kueneza uchochezi wa vita na chuki inayosababisha ubaguzi au kuibua migogoro na utumizi wa mabavu dhidi ya jamii nyingine. Pia, kwa mujibu wa sheria hizo, nchi zinatakiwa kuepuka propaganda zozote za vita au chuki zinazochochea vurugu za rangi, kidini, kikabila na kitaifa.

Jarida la Charlie Hebdo lilipochapisha vikatuni vya udhalilishaji na matusi dhidi ya Mtume Mtukufu (saw) na maeneo matakatifu ya Waislamu mwaka 2015, serikali za Magharibi zinazodai kutetea uhuru wa kujieleza sio tu hazikulaani kitendo hicho cha uvunjiwahi heshima matukufu ya kidini, bali zilikiunga mkono kwa nguvu zao zote. Kwa hakika, vitendo vya nchi hizo zinazodai kutetea uhuru wa kujieleza vinaonyesha wazi kwamba zina misimamo ya kindumakuwili kuhusu suala zima la uhuru wa kusema na haki za binadamu, na hulitumia vibaya kwa ajili ya kueneza chuki dhidi ya Uislamu na kufikia malengo yao haramu katika pembe tofauti za dunia.

Kwa mfano, hatua iliyochukuliwa karibuni na mtandao wa kijamii wa Instagram ya kufunga akaunti ya lugha ya Kifaransa ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwenye mtandao huo ni mfano wa wazi wa undumakuwili huo wa nchi za Magharibu kuhusiana na suala la uhuru wa kujieleza. Sababu ya kuchukuliwa hatua hiyo iliyo kinyume na misingi ya uhuru wa kujieleza ilihusishwa na ombi lililotolewa na Kiongozi Muadhamu kwa vijana wa Ufaransa akiwataka wamuulize rais wao, Emmanuel Macron, maana ya uhuru wa kujieleza.

Mfano mwingine wa wazi wa kukiukwa misingi ya uhuru wa kujieleza katika nchi za Magharibi ni kesi ya kuhukumiwa Mmarekani mmoja katika jimbo la Iowa ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 16 kwa sababu tu ya kuchoma bendera ya mashoga. Sababu iliyotolewa na mahakama katika kuhalali uamuzi wake dhidi ya mtuhumiwa huyo ni kwamba alieneza chuki na kutoheshimu uhuru wa kujieleza.

Vile vile hatua ya nchi za Magharibi ya kupiga marufuku matangazo ya vyombo vya habari vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfano mwingine wa wazi wa kukiukwa uhuru wa kujieleza katika nchi hizo. Bila shaka suala hilo linakiuka wazi haki ya taifa la Iran ya kuwafikishia walimwengu sauti yake kuhusu masuala mbalimbali, na hivyo kuanikwa peupe nara za uongo na za hadaa za nchi hizo kuhusu suala la uhuru wa kujieleza, uhuru ambao nchi za Magharibi ikiwemo Ufaransa yenyewe, zinautumia vibaya kwa lengo la kuhalalaisha matusi na kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini.

Ni wazi kuwa licha ya kuwa uhuru wa kujieleza umeruhusiwa katika sheria za kimataifa lakini uhuru huo umeshurutishwa na kuheshimiwa haki za wengine, kulindwa usalama wa taifa, utulivu, nidhamu, usalama na maadili ya umma. Kwa msingi huo hatua za dharau, matusi, udhalilishaji na uvunjiwaji heshima matukufu ya kidini unaofanywa na jarida la Charlie Hebdo kwa uungaji mkono kamili wa serikali ya Ufaransa na nchi nyingine za Magharibi, haziwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kujieleza.

Ni kwa msingi huo ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikakemea vikali uzembe unaofanywa kwa makusudi na viongozi wa Ufaransa katika kukabiliana na madhihirisho ya chuki dhidi Uislamu na kuenezwa ubaguzi wa rangi katika majarida na magazeti ya Ufaransa. Viongozi wa Iran wanawabebesha moja kwa moja watawala wa Ufaransa dhima ya suala hilo na kuwataka wawawajibishe wahusika wa matusi na chuki hiyo. Wamewataka wawajibike ipaswavyo katika kukabiliana na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika nchi hiyo ya Magharibi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *