Kufuatia kauli ya mwanamfalme wa Uingereza Harry, ya kuungama kwamba aliua Waafghani 25 wakati wa vita nchini Afghanistan, maafisa wa serikali ya Taliban wametangaza kuwa hatua hiyo ya mwanamfalme huyo wa Uingereza ni uhalifu wa kivita.
Anas Haqqani, mwanachama mwandamizi wa Taliban, ameeleza katika ujumbe wa Twitter aliotuma kujibu matamshi ya mwanamfalme Harry wa familia ya kifalme ya Uingereza, ambaye amesema, alipohudumu jeshini nchini Afghanistan, “aliwafuta Waafghani 25 mithili ya zinavyofanywa kete za mchezo wa chesi”, ya kwamba: “wale uliowaua walikuwa binadamu na walikuwa na familia”.
Haqqani amesisitiza kuwa, kitendo cha mwanamfalme wa Uingereza ni uhalifu wa kivita na akaongezea kwa kusema: ukweli ni kwamba mbele ya macho ya wanajeshi wenu na viongozi wenu wa kisiasa, watu wetu wasio na hatia walikuwa mithili ya kete za mchezo wa chesi, lakini mlishindwa katika mchezo wenu huo”.
Bilal Karimi, msemaji wa serikali ya Taliban, naye pia ameandika jumbe kadhaa za Twitter akisema: “jinai hii haikomei kwa mwanamfalme Harry, kwani wavamizi wote katika historia walifanya uhalifu sawa na huo na Waafghani hawatasahau kumbukumbu ya jinai hizi.”
Harry anayejulikana kama “Duke wa Sussex”, akiwa ni mtoto wa mwisho wa Charles III, mfalme wa sasa wa Uingereza; na ambaye kwa muda sasa amejiweka nje ya mduara wa ukoo wa kifalme, na huku akiandamana na mkewe Mmarekani anafanya mahojiano na kutoa nyaraka mbalimbali za kuchafua sura ya familia ya kifalme ya Uingereza, amekiri kuua watu wasiopungua 25 wakati wa vita vya Afghanistan.
Gazeti la Kiingereza la Telegraph limechapisha habari hiyo na kuandika: Harry, mwenye umri wa miaka 38, katika kitabu chake kiitwacho “Spare”, kitakachochapishwa wiki ijayo, amesema, wakati wa duru ya pili ya kuwepo kwake katika vita huko Afghanistan, aliua watu wasiopungua 25″.
Kulingana na ripoti hiyo, Harry ameshiriki katika vita vya Afghanistan mara mbili, kati ya 2007 na 2008 kama askari wa nchi kavu na kisha kama rubani katika helikopta za mashambulizi za Apache kati ya 2012 na 2013.