Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amelalamikia vikao visivyoisha na vya kila mwezi vya Baraza la Usalama la umoja huo kuhusu faili la silaha za kemikali la Syria na kusema kuwa, vikao hivyo vinafanyika kiudanganyifu kwa manufaa ya baadhi ya nchi za Magharibi.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Dmitry Polyanskiy akisema hayo kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kadhia ya silaha za kemikali za Syria na kuongeza kuwa, inasikitisha kuona kuwa, mwaka huu wa 2023 nao umeanza kwa kikao cha kimaonyesho tu kuhusu faili la silaha za kemikali za Syria.
Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameongeza kuwa, vikao hivyo havina maana yoyote na vinafanyika kwa ajili ya kufanikisha tu malengo ya baadhi ya madola ya Magharibi. Amesema, hatuoni chochote kwenye vikao hivyo isipokuwa kuongezeka malalamiko tu.
Russia na wanachama wengine wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza mara chungu nzima kuwa, kuzungumziwa suala la silaha za kemikali za Syria kila mwezi ni kwa ajili tu ya kulinda maslahi ya kisiasa ya ndani ya baadhi ya nchi za Magharibi.
Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa vile vile amesema, Moscow haioni faida yoyote ya kuendelea kushiriki kwenye vikao hivyo kwani mara zote Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kupiga Marufuku Silaha za Kemikali amekukwa akitafuta visingizio hivi na vile vya kutoshiriki kwenye vikao hivyo na kila mwezi anatoa ripoti hiyo hiyo kuhusu silaha za kemikali za Syria bila ya kuonesha nia yoyote ya kuimaliza kadhia hiyo.
Madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani muda wote yanatumia vibaya taasisi za kimataifa kwa ajili ya kuyashinikiza mataifa huru ambayo yanakataa kuburuzwa na madola hayo ya kiistikbari.