Kongamano la kitaaluma la wanazuoni wa Ulimwengu wa Kiislamu limefanyika jijini Dar es Salaam kwa kuhudhuriwa na wanafikra kutoka Tanzania na Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB katika kongamano hilo wahadhiri wa vyuo vikuu na watafiti waliwasilisha makala zenye anuani “umuhimu wa maelewano kati ya wanazuoni wa Ulimwengu wa Kiislamu na kuepukana na kulaaniana na kukufurishana”, “mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu; matumaini, changamoto na masuulia”, “kuvutiwa vijana na Uislamu na Njia Mbili za Jihadi ya Ukufurishaji au Jihadi ya Muqawama”, “Palestina na Quds Tukufu maudhui muhimu zaidi ya Ulimwengu wa Kiislamu”, “Piganio tukufu la Palestina, mhimili wa umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu” na “Ulimwengu wa Kiislamu na Ukufurishaji tokea jana hadi leo”.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ali Taqavi, Mkuu wa ofisi ya uwakilishi wa kikanda ya chuo kikuu cha kimataifa cha Jaamiatu al-Mustafa Al-Alamiya nchini Tanzania, amesema lengo la kufanyika kongamano hilo ni kuonyesha ulazima wa kuwepo umoja katika Umma wa Kiislamu kupitia Aya na Hadithi.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Taqavi ameongeza kuwa, kongamano hilo linafuatilia malengo kadhaa kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa kitu kimoja na kushirikiana zaidi jamii za Kiislamu.
Mkuu wa ofisi ya uwakilishi ya Jaamiatul-Mustafa Al-Alamiya nchini Tanzania amebainisha kuwa, kusaidia kuhuisha na kupanua utamaduni na mafundisho ya Kiislamu, kutetea utukufu wa Qur’ani Tukufu na Sunna za Bwana Mtume (SAW), kufanya juhudi za kujenga uelewa na mafahamiano zaidi kati ya maulamaa, wanafikra na viongozi wa kidini wa ukanda huo katika nyanja za kiitikadi, kifiqhi, kijamii na kisiasa, kueneza fikra ya kukurubiana kati ya wanafikra na wasomi wa eneo hilo na kuufikisha mtazamo huo kwa umma wa Kiislamu sambamba na kuwatanabahisha Waislamu juu ya njama za kuleta mfarakano za maadui wa Uislamu, na vilevile kuondoa hisia hasi na shubha miongoni mwa wafuasi wa madhehebu za Kiislamu ni miongoni mwa malengo muhimu ya kongamano hilo la kuwakurubisha pamoja Waislamu.